Breaking News

Adrian Mgaya wa Mlimani TV Mshindi wa Jumla EJAT 2020

Adrian Nicholaus Mgaya wa  Mlimani TV ameibuka mshindi wa jumla wa Tuzo za Umahiri za Uandishi wa Habari Tanzania(EJAT) 2020.

Adrian aliwapiku washindi wengine watatu -Veronica Romwald Mrema  wa  Matukio na Maisha blog, Sanula Renatus Athanas  wa Nipashe  na Alfred Lasteck Mushi wa  Habari Leo kutwaa  ushindi wa jumla katika kilele cha EJAT katika  ukumbi wa  Kituo cha Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Mgeni rasmi wa Tuzo hizo   Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mstaafu, Joseph Warioba, alisoma jina la Adrian  baada ya  kukamilika kutajwa kwa washindi  wa makundi mengine ya tuzo hizo.

Adrian  alishukuru kwa kupata ushindi  huo na  kuwataka vijana wengine  wasichoke kujaribu  ili kuweza kupata mafanikio.

Akiwa dhahiri amehemewa kwa ushindi huo, alisema yeye hakutarajia kupata ushindi huo na hakuweza kuendelea kuzungumza zaidi baada ya kushukuru pia kituo chake cha Mlimani TV .

Katika Tuzo hizo  mtoto wa miaka  13 Hadija Halifa Sadiki   aliyeripoti kwa kituo cha Ujerumani cha DW alipewa Tuzo pia ingawa  aliibuka mshindi wa  tatu katika kundi la ubunifu na maendeleo   kwa ruinga. 

Hadija alipiga picha pamoja na mgeni rasmi Waziri Mkuu Warioba, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari, Jaji  mstaafu Robert Makaramba na  Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT  Kajubi Mukajanga ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania

Adrian Nicholaus Mgaya wa  Mlimani TV,  mshindi wa jumla wa Tuzo za Umahiri za Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2020.

No comments