Viongozi Wa Ccm Na Serikali Toeni Elimu Kwa Wananchi Juu Ya Chanjo Ya CORONA Na Ulipaji Wa Tozo Nchini "KALIMA"
WITO umetolewa kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake tatu (Uvccm, Uwt na Wazazi) wakishirikiana na serikali kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuchanjwa chanjo ya uviko 19 na ulipaji wa tozo mbalimbali katika huduma zinazotolewa na serikali iliyoanza hivi karibuni.
Hayo yalisemwa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu. Gilbert Kalima, akiwa ziarani Mkoa wa Kigoma wilayani Uvinza pamoja na kujitambulisha kwao baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kumteua kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya CCM ambapo pia aliwahimiza viongozi wa CCM na jumuiya zake kusimamia uhai wa chama hicho kwa kuhakikisha wanalipa ada na kuongeza wanachama wapya.
"Viongozi wenzangu wa CCM na jumuiya awali ya yote nimeleta salamu ya msimamo wa chama chetu kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa chama, Ndugu, Daniel Chongolo, juu ya kuhimiza viongozi CCM na serikali kuanzia ngazi ya matawi, vijiji, vitongoji, mitaa, kata, wilaya, mikoa na kitaifa kuhakikisha mnasimamia ilani ya CCM ya mwaka 2020 - 2025 inatekelezwa kote nchini, hivyo nanyi viongozi wa Mkoa wa Kigoma nawapa salamu hii;
"Lakini pia kuwasisitiza ndugu zangu viongozi wa CCM na jumuiya zake zote tatu ambazo ni jumuiya ya Wazazi, Uwt na Uvccm mkishirikiana na serikali kuwaeleza wananchi juu ya umuhimu wa kuchoma sindano ya chanjo ya corona (Uviko 19) ili kujikinga na ugonjwa huo ili wananchi wafanye maamuzi yaliyo sahihi" alisema Kalima.
Aidha katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi, Kalima, aliwaambia viongozi hao wa chama na serikali kushirikiana kutoa elimu ya ulipaji wa Tozo inayokatwa na serikali kwa wananchi iliyoongezwa katika baadhi ya huduma katika bajeti ya mwaka huu iliyoanzia mwaka wa fedha kuanzia mwezi wa saba mwaka huu.
"Ndugu zangu viongozi wa CCM, jumuiya zote na serikali niwaombe katika maeneo tunayoishi tutenge muda wa kutoa elimu kwa wananchi ili waelewe umuhimu wa tozo hizi ambazo zikikatwa kwenye huduma au bidhaa wanazochukua zinakwenda moja kwa moja kuingia katika mfuko wa serikali kuu;
"Kuimarisha uchumi wa taifa ambao tupo uchumi wa kati lakini pia fedha hizo zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo barabara, afya, elimu na huduma nyinginezo hivyo amewataka viongozi hao kutoa ufafanuzi wa kutosha kwa wananchi hao ili wapate uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa kulipa kodi pamoja na tozo hizo zilizoanzishwa katika baadhi ya huduma ambazo hapo awali zilikuwa hazijawekwa." alisema Kalima.
Akiwa wilaya ya Uvinza katika shule ya sekondari ya Chumvi inayosimamiwa na jumuiya ya wazazi aliwahimiza viongozi wa CCM, jumuiya zote, serikali na walimu kutoa elimu bora, malezi na kuwafundisha maadili wanafunzi wa shule zote ili kuja kuandaa vijana hao kuja kuwa viongozi na wasimamizi bora katika siku zijazo, amewakumbusha viongozi na wanachama wa CCM na jumuiya zake kujiandaa kuelekea uchaguzi wa kichama kwa mwakani 2022 kwa kuchagua viongozi bora na siyo bora kiongozi.
Katika ziara hiyo pia Katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi, Kalima, atashiriki katika vikao mbalimbali katika wilaya zote za Mkoa wa Kigoma katika kutatua changamoto za migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara katika mali za jumuiya hiyo ikiwemo mipaka na usimamizi wa shule hizo.
Katika msafara wake, Katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi, Ndugu, Gilbert Kalima, ameongozana na Mkuu wa kitengo cha Milki kutoka Makao Makuu ya CCM, Ndugu, William Obimbo na Mwanasheria wa jumuiya ya wazazi, Ndugu, Beatus Mafuru.
Na. Elisa Shunda
No comments