Wastaafu 10,000 Wa Psssf Waliokuwa Wanadai Malimbikizo Ya Pensheni Ya Mkupuo Na Ile Ya Kila Mwezi Wamelipwa Bilioni 880
MFUKO wa Hifadhi ya
Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF) umefanya malipo ya zaidi ya shilingi
bilioni 880 kwa wastaafu elfu 10,000 ambao walikuwa wanadai malimbikizo ya
pensheni ya mkupuo na ya kila mwezi, Meneja Kiongozi wa Mfuko huo Bi. Eunice
Chiume amesema.
Amesema malipo hayo
yamefanyika katika kipindi cha mpito kilichotolewa na serikali kuanzia
Agosti 2018 hadi Februari 2019 hii ikiwa ni chini ya mwaka mmoja tangu Mfuko
huo uanze kutekeleza majukumu yake Agosti 1, 2018 baada ya serikali kuunganisha
Mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii, ambayo ni PSPF, LAPF, PPF na GEPF.
“Ili kuhakikisha
PSSSF inatoa huduma bora na za haraka, imefungua ofisi mikoa yote Tanzania bara
na Visiwani na tunatoa wito sasa, kwa wale wastaafu takriban elfu 10,500 ambao
bado taarifa zao hazijahakikiwa wafike kwenye ofisi zilizo karibu nao ili
kukamilisha zoezi hilo muhimu linalofanyika kila mwaka.” Alisema Meneja huyo
kiongozi wakati akizungumza na waendesha bloggers na waendesha mitandao ya
kijamii kwenye ofisi za PSSSF, barabara ya Ohio jijini Dar es Salaam Juni 13,
2019.
Alisema uhakiki wa
wastaafu sio kitu kipya ingawa mwaka huu zoezi hilo lilionekana kama ni geni.
“Lengo la uhakiki
ni kuupa Mfuko fursa ya kufanya malipo kwa usahihi na kwa mtu anayepaswa
kulipwa kwani taarifa zinaweza kubadilika ikiwa ni pamoja na zile za kibenki
huenda muhusika akahama kutoka benki moja kwenda nyingine, mabadiliko ya
wategemezi lakini haka kifo pia.” Alifafanua Bi. Chiume.
No comments