Breaking News

Profesa Lipumba Achambua Bajeti Ya Serikali 2019/20

MWENYEKITI wa Chama cha wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amekosoa Bajeti ya serikali ya mwaka 2019/2020 baada ya kusema bado serikali haina nidhamu kwenye matumizi ya Bajeti.

Akizungumza makao makuu ya chama hicho buguruni jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa maoni ya chama hicho juu ya Bajeti ya serikali ya Mwaka 2019/2020  iliyowasilishwa Bungeni na  Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango.

Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Uchumi alisema bado kumekuwa na kutokuwa na nidhamu kwenye utekelezaji wa Bajeti  na kupelekea mipango mingi ya nchi kukwama.

Alisema licha ya kuwepo kwa sheria zinazohusu bajeti lakini bado serikali imeshindwa kuwa na nidhamu kwenye utekelezaji wa bajeti husika.

“Bajeti zinasomwa Bungeni lakini bajeti inayotekelezwa na serikali haiendani na  bajeti iliyopitishwa na Bunge,kutokana na serikali kutekeleza miradi mbali mbali nje ya Bajeti iliyopitishwa na Bunge”Alisema Profesa Lipumba.
Msomi huyo ametolea mfano wa miradi iliyotekelezwa na Serikali ambayo haikupitishwa na Bunge ni Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma, Manunuzi ya Korosho pamoja na miradi wa kufua umeme mto Rufiji.

Alisema kitendo cha serikali kutekeleza miradi kinyume cha bajeti kinaathiri maendeleo na kinaleta picha mbaya ya kutokuwepo na nidhamu ya usimamizi wa bajeti.

Aidha Profesa Lipumba aliongeza kuwa licha ya Bajeti kupitishwa bungeni lakini bado fedha za maendeleo zilizopitishwa hazitolewi zote.

“Fedha za mipango ya maendeleo zilizopotishwa kwenye Bajeti hazitilewi zote,kwa mfano Wizara ya Madini kwenye mwaka 2018/2019 Bunge lilipitisha Bilioni 2.9 kwa ajili ya mipango ya maendeleo,lakini matokeo yake serikali ilitoa Milioni 100 tu,” Alifafanua Profesa Lipumba.

Aidha,Profesa Lipumba ameishauri serikali kuweka wazi miradi mbali mbali inayojengwa na serikali ili wananchi waweze kufahamu uzuri wa miradi hiyo na hasara zake.

No comments