Bodi Yampongeza Dkt. KIJAZI Kuchaguliwa Makamu Wa Tatu Wa Rais Wa WMO
Bodi ya Ushauri ya
Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imempongeza Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa
TMA na katibu wa hiyo kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa makamu wa tatu wa Rais
wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Akizungumzia
pongezi hizo na ushindi uliopatikana wakati wa kikao cha 55 cha Bodi,
mwenyekiti wa Bodi Dkt. Buruhani Nyenzi aliwasilisha pongezi za dhati kutoka
kwa wajumbe wote na kukiri kuwa nafasi iliyopatikana ni moja ya njia za kuzidi
kuipandisha Tanzania juu katika anga za kimataifa.
‘Bodi inatoa
pongezi za dhati kwa Dkt. Kijazi kwa kuchaguliwa kushika nafasi ya juu WMO, kwa
kuwa kupitia nafasi hiyo Tanzania inazidi kupanda juu katika anga za
kimataifa’. Aliongea Dkt. Nyenzi
Mwenyekiti huyo
aliendelea kuwakumbusha washiriki wa kikao hicho kuwa mafanikio ambayo Tanzania
imeyapata yanachangiwa na mambo mengi. Alisema jambo la kwanza na la muhimu ni
sifa za Dkt. Kijazi kama mgombea wa nafasi hiyo, pili kukubalika na kukua kwa
diplomasia ya Tanzania nje ya nchi na tatu sifa nzuri za Watanzania ambao
wamewahi kufanya kazi WMO akiwemo yeye mwenyewe.
Aidha, Dkt. Nyenzi
alionesha furaha yake namna ambavyo TMA inafanya kazi kwa umoja na upendo baina
ya wafanyakazi, akitolea mfano mapokezi yaliyofanywa na wafanyakazi kwa
kiongozi wao ambaye ni Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi
alichaguliwa kuwa makamu wa tatu wa Rais wa WMO kwenye mkutano wa 18 wa shirika
hilo uliofanyika jijini Geneva, Uswisi tarehe 03-14 Juni 2019 kwa kipindi cha
miaka minne, akiwa mwanamke na makamu wa tatu wa Rais wa kwanza kutoka nchi
zinazoendelea hususani nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.
IMEANDALIWA NA;
OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA)
No comments