Breaking News

Wajumbe Wa Bodi Mpya Ya TANROAD Wakagua Miradi Mbalimbali Inayoendelea Jijini Dar.

WAKALA wa Barabara nchini (TANROADS) umesema kuwa miaka mitatu ijayo jiji la Dar es Salaam litakuwa lenye kupendeza na kufanana kama ulaya baada ya miradi mikubwa mitano inayoendelea kujengwa kukamilika.

Miradi hiyo inayoendelea kujengwa jijini Dar es Salaam ni pamoja na Ubungo Interchange, ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III) katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA TB III).

Mingine ni ujenzi wa daraja jipya la Selander na barabara unganishi, upanuzi wa barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kibaha kuwa njia nane na Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya ziara ya wajumbe wa bodi mpya ya TANROADS kutembelea miradi inayosimamiwa na wakara huyo jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale alisema jiji hilo litakuwa la tofauti sana.

“Mi kazi yangu ni kujenga ili jiji liiwe kama ulaya vile, si mmeona Aiport nani amesafiri nje ya nchi, ile Terminal III inayojengwa imefanana na viwanja vingi duniani,” alisema Mhandisi Mfugale.

“Miaka mitatu ijayo maana yake 2022 litakuwa imebadilika sana, tutegemee foleni siyo nyingi, tutegemee jiji litakuwa limependeza zaidi, mmeona wenyewe sasa hivi tunajenga SGR juu kwa juu, reli kutoka bandarini tunategemea kwenda hadi Mwanza,” aliongeza. 
Ubungo Interchange 
Akizungumzia mradi huu, Mhandisi Mfagale alisema kuwa matarajio ni kwamba Desemba mwaka huu kwa upande wa Morogoro Road utakuwa umekamilika.

“Tumeanza ujenzi 2017 na tutamaliza ujenzi kwa sehemu kubwa Desemba mwaka huu, niseme tu kwa maka huu mwishoni Interchange kwa Morogoro Road itakuwa imekamilika, alisema Mhandisi Mfugale.

Mhandisi huyo alieleza kuwa kwa Interchange upande wa Barabara ya Mandela/Sam Nujoma unatarajia kukamilika mwezi Mei mwakani 2019 na kusema kuwa kwa hatua ambayo mradi huo umefikia haina shaka utakamilika kwa muda uliopangwa.

Alisema baada ya kusaini mkataba mkataba wa Machi 22, 2017, Mkandarasi alianza kazi rasmi mwezi Mei 2017. Kazi alizoanza nazo ni pamoja na matayarisho na kuhamisha miundombinu ya maji, umeme, gesi na ya mawasiliano iliyokuwepo ndani ya eneo la ujenzi.

Alisema baada ya kuhamisha miundombinu hiyo hatua iliyofikia ni kwamba ujenzi wa barabara za pembeni imekamilika kwa asilimia 80 na magari yameshahamishiwa huko ili kupisha ujenzi wa madaraja ya juu.  

Kwa upande wake Meneja Mradi huo kutoka TANROADS Mhandisi Barakael Mmali, alitaja kazi zinazoendelea katika eneo hilo la ujenzi, baadhi ya kazi hizo ni pamoja na upanuzi wa madaraja kwenye barabara za Nelson Mandela na Sam Nojuma ambao umekamilika kwa asilimia 70.

Nyingine ni Ujenzi wa barabara za pembeni kilometa 1.5 zilizokamilika kwa asilimia 80, ujenzi wa misingi ya daraja (Piles) zenye kipenyo cha m.0.9m na urefu kati ya mita 22 ambapo nguzo 120 zimeshajengwa.

Mmali aliendelea kubainisha kazi nyingine kuwa ni ujenzi wa vitako juu ya misingi ya daraja ambapo vitajengwa jumla 39, hivyo kwamba maandalizi ya ujenzi wa vitako vitano unaendelea na ujenzi wa nguzo za daraja kutoka kwenye vitako kwenda juu ya ardhi ambapo jumala ni 64 hivyo maandalizi yanaendelea.

Mhandisi Mmali alisema hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umedikia asilimia 25 na umepangwa kukamilika mwishoni mwa Desemba 2020.

Mradi huu wenye thamani jumla ya sh.bilioni 247 kati ya fedha hizo sh.bilioni 200 ni mkopo kutoka  Benki ya Dunia ndani ya mradi wa mkuu wa kuboresha usafiri jijini Dar es Salaam uitwao “Dar es Salaam Urban Transport Improvement project” huku serikali ya Tanzania ikichangia sh.bilioni 47.

Daraja la Selander
Alisema ujenzi wa daraja hilo unaendelea vizuri na kueleza kuwa hatua iliyofikia sasa ni ujenzi wa daraja la muda ambalo limefikia urefu wakilometa 1.05.

Alisema daraja hilo litatumika kusafirishia vifaa wakati wa ujenzi wa daraja lenyewe.

“Na mmeona progress kwa sasa ni asilimi 5.3 na tulitegemea iwe 5.2 kwa hiyo mkandarasi yupo sawa , kwa hiyo atamaliza kazi kwa muda uliopangwa, tumeangalia na mmeona jinsi zile nguzo anavyoziingiza na mashine zake zote zimeshafika kwa hiyo hatuna wasi wasi nae,” alisema Mhandisi huyo.

Daraja hilo lenye urefu wa meta 1,030 na upana  wa meta 20.5 litakuwa na njia 4 za magari na njia 2 za watembea kwa miguu, na litajengwa pamoja na barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 5.2
Mradi huu utagharimu shilingi Bilioni 256 zilizotolewa kwa mkopo nafuu kutoka Jamhuri ya Korea kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF) na Serikali ya Tanzania.
Daraja hilo lintarajia kudumu kwa muda wa miaka 100 na litajengwa bila kuathiri nyumba zilizopo kando ya barabara za Kenyatta na Toure ambazo miongoni mwake wanaishi Mabalozi. 
 Viwanja vya ndege.


Mhandisi Mfugale alisema kuwa TANROADS pia imepewa kujeinga mradi wa viwanja vya ndege ambapo kwa sasa wanasimamia ujenzi wa ujenzi wa jengo la Terminal III. 

Alisema tangu 2013 lilikuwa linajengwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) lakini TAA 2017 waliwakabidhi kuujenga mradi huo. 

Alsema hadi sasa mradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na kwa mujibu wa mkataba mradi utakamilika Mei 31, 2019 kwani kila kitu ni kama kimekamilika kazi iliyopo ni kumalizia kupaka rangi na kufanya usafi wa jengo.

Aliongeza kuwa jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kubeba abiria milioni 6 kwa mwaka tofauti na Terminal II ya sasa inayochukua abiria milion 2 kwa mwaka.

Barabara 8 Kimara hadi Kibaha

Alisema mradi huu ulipangwa kufanyika kwa miezi 30 kuanzia Julai 21,2018 ambapo unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 141.56 Fedha zote kutoka serikali ya Tanzania na unasimamiwa kwa asilimia na TANROADS wenyewe.

Mradi huo Utakuwa na umbali wa kilomita 19.2 na utahusisha upanuzi wa njia nane, njia mpya kabisa sita zitajengwa, tatu kwenda Dar es Salaam na tatu kwenda Morogoro na mbili zilizokuwepo.

“Lakini za zamani zile za katika kati tutaziboresha zaidi ili ziungane na hizo barabara mpya zinazojengwa,” alisema Mhandisi Mfugale.

Mradi huo muhimu ukikamilika utasaidia kupunguza msongamano mkubwa wa Magari takribani 50,000 yanayopita katika barabara hiyo kila siku .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi Dk. Dalmas Nyaoro alikiri kuridhishwa na miradi hiyo inavyoendelea, lakini aliishauri TANROADS kuwa karibu na wakandarasi ili kuwasimamia na kuhakikisha wanajenga miradi hiyo kwa ufanisi.

“Ushauri wetu kwa tanroad ni vizuri wakawepo wakati wakandarasi wanajenga ili kujiridhisha kwamba hiki walichosema watajenga ndiyo hicho wanchojenga,” alisema Dk. Nyaoro.

Alieleza kuwa kama hawatakuwepo tatizo katika mradi likitokea hawawezi kujua kama tatizo lilikuwa ni usanifu ama ni mkandarasi.

“Ni kwamba TANROADS  wawe na mtu wao kwenye eneo la mradi ambaye anasimamia kwa karibu na kuhakikisha kwamba kile kinachotakiwa ndicho  kinachofanyika,” aliongeza.

Alisisitiza “Wanatakiwa kuwa makini hususani upande wa ujenzi wa msingi kwani ukishaweka kitu chini ya ardhi huwezi ukajua chini kuna nini kama hukuwepo, huku juu unaweza ukajua, lakini chini ya ardhi ni vizuri kujihakikishia wakati wanajenga,”.

Aidha alipongeza ujenzi wa mradi wa barabara za juu unaoendelea eneo la Ubungo kwa kusema kuwa kazi inakwenda vizuri na kueleza kuwa ukikamilika utamaliza tatizp la foleni. 

No comments