Breaking News

Ado Shaibu Kufungua Kesi Kupinga Uteuzi Wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha ACT-Wazalendo Ado Shaibu, amemwelekeza Wakili Fatma Karume kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Shaibu amesema kuwa amechukua hatua hiyo kutokana na uteuzi huo kutofuata masharti ya Katiba.

“Kwenye kesi hiyo, nimemwelekeza wakili wangu (Fatma Karume ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)) kuwa mdaiwa awe Ndugu John Pombe Magufuli na Ndugu Kilangi Mwanasheria Mkuu wa Serikali aunganishwe,” alisema Shaibu.

Alisema sababu ya Kumuweka Rais Magufuli kama mdaiwa ni kutokana na yeye kuwa mwenye mamlaka ya uteuzi ambaye anatakiwa kulinda na kuifuata katiba.

Aidha alisema kuwa suala hilo tayari wakili Fatma Karume amekwishaliingiza kwenye mchakato wa kimahakama na kwamba kinachosubiriwa ni kupangiwa Jaji wa kuisimamia na tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Sababu ya Dk. Kilangi Kupingwa.

Shaibu alisema kuwa Katiba imeweka masharti maalumu ya uteuzi wa mtu wa kushika nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Ibara ya 59 (2) imeweka masharti kuwa mtu anayeteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu ni lazima awe mtumishi wa umma mwenye sifa za kuwa wakili kwa miaka 15,” alieleza Shaibu.

Alibainisha kuwa kwa mujibu wa utafiti aliofanya amebaini kuwa Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali Dk. Kilangi hana sifa hizo.

Alifafanua kwamba utafiti huo umebaini kuwa Dk. Kilangi amekuwa na sifa ya kuwa wakili kwa miaka saba tuu, na pia hana sifa ya kuwa mtumishi wa umma kwa miaka hiyo.

Dk. Kilangi aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwezi Februali, 2018.

No comments