Maalim SEIF: Waraka Mzito KKKT Umemfariji

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amelipongeza Baraza
la Maaskofu la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kutoa waraka
mzito wa ujumbe wa Sikukuu ya Pasaka.
Waraka huo ulitolewa mwishoni wa wiki iliyopita ambao mbali na
kuzungumzia masuala ya kiroho, umetaja changamoto tatu na kuzifikisha kwa
waumini wake “ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake.”
Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la “Taifa
Letu Amani Yetu” na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini ni hali ya
kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mtambuka likiwamo suala la
Katiba Mpya.
Akizungumza leo Machi 26, 2018 jijini Dar es salaam wakati
akisoma maazimio manne ya Kamati ya Utendaji ya Taifa ya chama hicho
iliyokutana leo, Maalim Seif amesema anafarijika kuona viongozi wa dini
wanakemea mambo ambayo hayaendi sawa nchini.
"Nimefarijika kuona viongozi wa taasisi za dini
wakizungumza pale ambao wanaona mambo hayaendi sawa. Tusitafsiri kwamba
wanafanya siasa, hapana ni haki yao kukemea, "amesema Maalim Seif.
Amesema angetamani kuona viongozi wengine wa dini wakionyesha
misimamo kama maaskofu hao.
Na Kelvin Matandiko Mwananchi
No comments