Waziri Lukuvi Amjibu Sumaye Sakata La Mashamba
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Mhe William Lukuvi amesema mtu yoyote asiyelipa kodi ya ardhi na
kuendeleza ardhi hiyo, ni sababu tosha ya kunyang'anywa ardhi hiyo pamoja na
kufutiwa hati ya umiliki kwa kuwa anaingizia hasara serikali
Waziri Lukuvi amebainisha hayo ikiwa
imepita siku moja tokea kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa awamu ya tatu, Mh.
Fredrick Sumaye kudai chanzo cha kupokonywa shamba lake ni siasa tu za yeye
kuhama chama cha CCM na kwenda kuupa nguvu upinzani.
Akiongea kuhusu mashamba na viwanja
kuchukuliwa Waziri Lukuvi amesema,
"Kila mtu atambue iwe ni kiwanja
au shamba kama unatabia ya kutolipa kodi ya ardhi ni sababu tosha ya wewe
kunyang'anywa shamba lako au ardhi unayomiliki.
"Imejitokeza kwa watu wachache
kuchukua ardhi kubwa kwa miaka mingi kuliko hata uwiano wa uendelezaji wa ardhi
hiyo, kwa mfano kuna hati moja hapa ambayo inapigiwa kelele tokea mwaka 1939
imekuwa ikitembea mikono mwa watu. Sasa miaka ile watu walikuwa wachache
unapokwenda kuchukua ardhi ya kijiji hekari elfu 60 kwa mfano hivi sasa
wananchi utakuwa umewaachia kitu gani?" Amesema Lukuvi
Pia Waziri Lukuvi amesema imekuwa
kawaida ya baadhi ya watu wanapowahi maeneo huwa wanakimbilia kuchukua
sehemu zenye manufaa makubwa kwa upande wao na mwishowe wanashindwa kuendelezaa
maeneo hayo kama walivyoyakimbilia.
"Unawahi kuchukua sehemu zenye
manufaa kama mto, ardhi inayolimika, sasa unachukua hekari zote hizo halafu
huliendelezi mwishowe shamba hilo hilo tunalikuta Benki umelikopea fedha. Kisha
umepata fedha hizo unakwenda kujengea 'apartment' sehemu nyingine na kule
wananchi wanalimezea mate.Serikali wanatumia nguvu kubwa sana kutuliza wananchi
wasivamie hilo shamba , halilimwi, serikali hatupati kodi", alisisitiza
Lukuvi.
Kwa upande mwingine, Waziri Lukuvi
amesema serikali imekuwa na huruma kwa miaka mingi kwa wananchi wake lakini
serikali ya uongozi huu wamekubaliana kila mtu afuate sheria anazo paswa.
No comments