Mkojo Wa Agnes Masogange Wazua Kizaa Zaa Mahakamani.
Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia
Mkuu wa Serikali, Elias Mulima, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa
sampuli ya mkojo wa msanii Agnes Gerald maarufu kama Deal ama Masogange (28)
umebainika kuwa na dawa ya kulevya aina ya heroin.
Akitoa ushahidi leo Jumatano
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, shahidi huyo wa kwanza wa upande
wa mashtaka, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula, ameiambia
mahakama kuwa mnamo February 15, 2017 askari wawili kutoka Jeshi la Polisi
Tanzania, Koplo Sospeter na WP Judith, walimfikisha Masogange ofisini kwake kwa
lengo la kumfanyia vipimo vya mjono wake.
Alisema baada ya kuwapokea,
alimsajili Masogange na kumpa namba ya maabara 446 /2017 na kisha kuwakabidhi kifaa
maalum kwa ajili ya kuweka sampuli ya mkojo.
Alidai baada ya kupokea sampuli
ya mkojo ya Masogange alifanyiwa uchunguzi kwa kutumia kemikali na kubaini kuwa
mkojo wake una chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroin ambazo kwa
kitaalamu zinajulikana kama Diacety Imophine.
Aidha, alisema uchunguzi zaidi
ulibaini chembechembe za dawa nyingine ya kulevya aina ya Oxazepam.
Shahidi huyo alidai baada ya
kufanya uchunguzi huo, aliandaa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na sampuli hiyo
ya mkojo ambapo aliisaini yeye mwenyewe na kuthibitishwa na kaimu mkemia mkuu
wa serikali.
Shahidi huyo alimtambua
Masogange kwa ndiye aliyepelekwa kuchukuliwa sampuli hiyo ya mkojo ofisini
kwake.
Pia alidai anaweza kuitambua
taarifa hiyo ya uchunguzi kutokana na kuwepo kwa saini yake, muhuri wa moto wa
maabara ya mkemia mkuu wa serikali. Pia ameomba mahakama kupokea vitu hivyo
kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.
Hata hivyo, mawakili Nehemiah
Nkoko na Reuben Simwanza ambao wanamtetea Masogange wamepinga taarifa hiyo ya
uchunguzi wakitaka isipokelewe na mahakama kwa madai haijakidhi vigezo vya
sheria.
Nkoko amedai utaratibu wa
kisheria haukufatwa kabla ya mtuhumiwa aliyeko chini ya polisi kufanyiwa
uchunguzi wa kitabibu, kwa kuwa ofisa wa polisi alitakiwa kuwasilisha maombi
mahakamani ndipo amri ya kupimwa itolewe.
Amesema katika ushahidi wake
mkemia huyo hajaeleza kama ofisa wa polisi alipeleka amri ya mahakama kutoka
mahakama yoyote ile.
"Ripoti
ipo kinyume na sheria, mahakama ina njia moja tu nayo ni kuikataa na sio
kuikubali. Sheria ipo wazi, tunaomba mahakama ikubali pingamizi letu na kukataa
kupokea taarifa hiyo," alisema.
Naye Wakili Simwanza alidai
ripoti hiyo ikitazamwa inataja fomu nyingine ya ombi la Jeshi la Polisi kwenda
kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kufanya vipimo.
Amedai ripoti hiyo ipo yenyewe
bila ya kuambatanishwa na fomu maalum inayotumiwa na polisi kupeleka sampuli
hivyo haiwezi kupokelewa na kutumika kama kielelezo.
Akijibu hoja hizo, Wakili
Kakula alidai mapingamizi hayo hayana mashiko wala miguu ya kusimamia.
Amedai fomu ambayo
haijaambatanishwa na ile ya mkemia mkuu ni vitu viwili tofauti na hata
uwasilishwaji wake unafanywa na watu wawili tofauti.
Alisema taarifa ya mkemia
inawasilishwa na mkemia na ile ya polisi inawasilishwa na polisi.
Kuhusu hoja ya sampuli ya
mkojo, Kakula alidai kifungu cha 63 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai
(CPA), kimeweka mazingira ambayo ofisa wa polisi atawasilisha maombi mahakamani
kuweza kuchukua sampuli.
Alisema iwapo mtuhumiwa
anakataa kuchukuliwa sampuli ya mkojo, hivyo atawasilisha ombi mahakamani ili
iweze kutolewa amri.
Kakula alisema katika pingamizi
lao upande wa utetezi haijaeleza kwamba mshitakiwa alikataa kupima,
akalazimishwa. Aliomba mapingamizi hayo yatupiliwe mbali.
Hakimu Mashauri ameahirisha
shauri hilo hadi Agosti 28, 2017 kwa ajili ya kutoa uamuzi wa ama kupokelewa
kwa taarifa hiyo ama la.
Masogange amefikishwa
mahakamani hapo akidaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya heroin kati ya
Februari 7 na 14, mwaka huu, katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jijini a Dar
es Salaam.
No comments