Serikali Kuunda timu ya Kukagua Viwanda Vyote Nchini
Serikali imeteua kamati maalumu
yenye kushirikisha wataalamu pamoja na wakuu wa mikoa wa kila mkoa,
itakayozunguka kukagua utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa, na kisha ndani
ya siku 15 itatoa maamuzi.
Imesema viwanda watakavyoshughulika
navyo ni vile vilivyobinafsishwa na ambavyo havifanyi kazi, lakini pia
kuhakikisha uzalishaji wa kiwanda husika kama ndio ulioruhusiwa.
Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Charles Mwijage alisema hayo jijini Dar es Salaam jana na kuongeza
kuwa wapo waliopewa viwanda kwa shilingi moja na wengine kwa Sh milioni 10,
vingine vikifanya kazi, vingine vikiwa havifanyi kazi iliyokusudiwa na vingine
kutokufanya kazi kabisa.
Alisema Kamati hiyo itafuatilia na
tayari ameandika barua kwa wakuu wote wa mikoa nchini, na kupewa hadidu za
rejea ili waweze kupitia kiwanda kimojakimoja kuhakikisha utendaji kazi
wake.
“Wakati Kamati hiyo ikikagua,
wakikiona kiwanda wanapiga simu kwake na kwa msajili wa hazina ili kwenda
kuhakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi na baada ya hapo Augusti 15 watafanya
maamuzi,”alisema.
Alisema yeyote aliyepewa kiwanda ni
lazima kifanye kazi na kwamba kama anayehusika ameshindwa, atafute mtu mwingine
ili kifanye kazi, la hasha ameagizwa akakichukue, kwani wapo watanzania ambao
ni vijana wanatafuta kazi wakihitaji kutolewa vijiweni na kupewa viwanda
waviendeshe na taasisi za kuwaelekeza zipo.
Alisema lengo la kubinafsisha viwanda
ni ili vizalishe bidhaa ambazo zitatumika nchini na nyingine ziweze kuuzwa nje
ya nchi na kuleta fedha za kigeni, vifanye kazi viweze kutoa ajira kwani
asilimia 65 ya idadi ya watu nchini n I vijana na wengi wao hawana ajira.
“Kuna viwanda vilivyobinafsishwa na
vinafanya kazi, hivyo hatuna shida navyo bali vile ambavyo havifanyi kazi,
kwani malengo yetu ni wote wenye viwanda vifaye kazi hata vile vilivyosimama
ili vikidhi malengo yaliyotakiwa,” alisema Mwijage na kuongeza kuwa
viwanda vingi vilitolewa kwa Shilingi moja na vingine hadi Shilingi milioni 10.
Alitoa wito kwa wakuu wa mikoa,
kukagua kiwanda kimoja baada ya kingine na hata kuhoji umiliki, hivyo mhusika
anatakiwa kuwa na nyaraka stahiki, kwani ubinafsishaji dhamira yake kubwa
ilikuwa ni kuwepo kwa ajira.
No comments