Rais Magufuli abariki uamuzi wa TCU kuvifungia vyuo 19
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewasili Jijini Dar es Salaam leo
tarehe 27 Julai, 2017 akitokea Mkoani Dodoma ambapo akiwa katika eneo la Tegeta
Wilaya ya Kinondoni amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake na
kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za
kukabiliana na kero na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
“Kwa
sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa Tegeta, nianze kwa kuwashukuru
sana, kwa kura nyingi mlizonipa ili niwe Rais wa Awamu ya Tano, nawashukuru
CCM, nawashukuru CHADEMA, nawashukuru CUF, nawashukuru ACT na hata wale ambao
hawana chama kwani wote kwa umoja wenu mlitanguliza maslahi ya Taifa na kumpa
kura mtu ambaye atalisaidia Taifa, na mimi nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote
na kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu ili Watanzania wote hasa wanyonge ambao siku
zote walikuwa wakionewa” amesema Mhe. Rais Magufuli
Baadhi ya juhudi alizozitaja
kufanyika tangu aingie madarakani ni pamoja na kuondoa ada kwa wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka
Shilingi Bilioni 371 hadi kufikia Shilingi Bilioni 483, kukabiliana na vitendo
vya rushwa na ufisadi na kulinda mali za umma hasa madini.
“Kwenye
madini tumeibiwa sana, nchi yetu ni kati ya nchi zinazoongoza kwa kuibiwa,
tumeibiwa kwa miaka 18, sasa imetosha” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuzuia udahili wa wanafunzi wote wa mwaka
kwanza katika vyuo vikuu 19 na kuzuia udahili wa wanafunzi wa kozi 75 katika
vyuo vikuu 22 kutokana na dosari zilizobainika wakati wa ukaguzi wa ubora vyuo
hivyo uliofanyika Oktoba 2016.
“Ndugu
zangu nchi hii ilishakuwa kila kitu hewa hewa, tumegundua wafanyakazi hewa
zaidi ya 19,500, kulikuwa na mikopo hewa ya wanafunzi, na naipongeza TCU kwa
kufungia baadhi ya vyuo kudahili wanafunzi, nafanya yote haya kwa ajili yenu,
nataka tuwe na nchi nzuri”amebainisha Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
27 Julai, 2017
No comments