NEC yatoa ufafanuzi uteuzi wa wabunge CUF
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imefafanua juu ya uteuzi wa wabunge wapya wa Viti Maalumu wa Chama cha Wananchi
(CUF).
Imesema kuwa imesikitishwa na
kushangazwa na taarifa za Baraza Kuu la Taifa la chama hicho kwamba tume hiyo
imekiuka kanuni zake katika uteuzi wa wabunge wanane wa chama hicho ili kujaza
nafasi za wazi zilizotokea hivi karibuni.
Aidha, imesema chama husika kilipewa
fursa ya kupendekeza na kilifanya hivyo, kabla ya NEC kuanika majina ya wabunge
wapya wa CUF katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yamo katika taarifa ya
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani aliyoitoa jana jioni, akizungumzia
tuhuma dhidi ya tume hiyo, inayodaiwa kukiuka kanuni katika uteuzi wa wabunge
wanane wa viti maalumu wa CUF.
Sehemu ya Taarifa ya CUF katika
mitandao ya kijamii inayoituhumu NEC inasema; “Kanuni walizojiwekea wenyewe Tume katika uteuzi wa watu wa kujaza
nafasi hizo zinasema uteuzi huo unafuata mpangilio wa majina, kama ulivyokuwa
umewasilishwa na chama husika wakati wa uteuzi wa wagombea wa ubunge wa viti
maalumu wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
“CUF
ilipeleka orodha yake ambayo haihusishi majina yaliyotangazwa, hivyo ndiyo
kusema hata kama hicho kinachoitwa kufukuzwa uanachama wabunge hao kingekuwa
halali (jambo ambalo si halali kama ilivyokwishaelezwa hapo juu), basi kwa
Kanuni za Tume yenyewe, watu wa kujaza nafasi hizo wasingekuwa hao waliotangazwa.”
Kailima, katika taarifa yake, alisema
taarifa zinazotolewa katika mitandao zikihusisha NEC kukihujumu chama hicho ni
za kushangaza na kwamba Baraza Kuu la Uongozi la CUF, linataka kuupotosha umma
kuhusu utekelezaji wa kazi za Tume.
“Chama
husika ndicho kinaweza kujua ni nani siyo mwanachama wa chama hicho kwa kipindi
cha kujaza nafasi wazi inapotokea,” alieleza Kailima na kuongeza
kuwa, kwa mujibu wa majina manane yaliyopendekezwa na CUF kujaza nafasi wazi za
wabunge wa viti maalumu ni miongoni mwa majina 55 yaliyowasilishwa na chama
hicho kwa barua yenye kumbukumbu Namba CUF/AK/DSM/ KM/003/1A/2015/14 ya
Septemba 28, 2015 iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff
Hamad.
No comments