KIGOGO WA SHIRIKA LA VIWANGO TANZANIA (TBS), AHUKUMIWA JELA MIAKA MITANO.
Baada ya kuachiwa huru siku ya Jumatano
na kukamatwa tena, jana aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango
Tanzania (TBS), Baptister Bitaho (54) amehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni
13.9 au kifungo jela miaka mitano baada ya kusomewa upya mashtaka na kukiri.
Bitaho alifikishwa tena katika mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jana asubuhi na kusomewa mashitaka nane likiwemo la kufanya
kazi nchini bila kibali na kutoa taarifa za uongo.
Bitaho ambaye ni Raia wa Burundi, alifutiwa
mashtaka yake, na baadae kukamatwa, alisomewa hukumu hiyo, na Hakimu Mkazi
Mkuu, Victoria Nongwa.
Akisoma hukumu hiyo Nongwa alisema kuwa
mahakama imesikiliza maombi ya pande zote mbili na kwamba katika kosa la kwanza
hadi la saba mshitakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh laki tano au kifungo jela
kuanzia miaka miwili hadi mitatu na kwamba kosa la nane mshitakiwa atatakiwa
kulipa faini ya Sh milioni 10 au kifungo jela miaka mitano.
Alisema, kwa taratibu zilizopo, baada ya
mshitakiwa kukutwa na hatia anatakiwa kupelekwa Uhamiaji na kurudishwa nchini
kwao ili aombe uraia wa Tanzania upya.
Kabla hukumu hiyo kusomwa, Wakili wa utetezi,
Aloyce Komba alidai kuwa mshitakiwa hakuwahi kuvunja sheria ya kijinai kwani
alikuwa mwaminifu na hakuwahi kutoa siri ya nchi licha ya ukimbizi wake.
Komba pia aliongeza kuwa, tangu mteja wake
apate kashfa hiyo, ameathirika kiuchumi kwa kuwa alitakiwa kustaafu miaka sita
ijayo lakini sasa anakosa mapato yake.
‘’Naomba mahakama isitoe adhabu kubwa kwa mteja
wangu kwani pamoja na ukimbizi wake, kutokana na vita za mara kwa mara
zinazotokea nchini Burundi, mshitakiwa ameanzisha kituo cha kulelea watoto
yatima wa Tanzania na Burundi hivyo amekuwa na msaada,’’alidai Komba.
Akimsomea maelezo ya awali (PH), baada ya
kukiri mashtaka yake, Mwendesha Mashitaka wa Uhamiaji, Method Kagoma alidai
wazazi wa Bitaho waliingia nchini mwaka 1958 na kisha kurudi tena mwaka 1972
huku yeye Bitaho akiwa mtoto mdogo.
Aliidai baada ya kukua, mshitakiwa huyo
alijiunga na elimu ya msingi, sekondari na vyuo hapa nchini na kwamba mwaka
2001 aliajiriwa na TBS kama mwanasheria.
Katika mashitaka yake inadaiwa Mei 19, mwaka
huu maeneo ya Ofisi ya Uhamiaji iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwa
mkimbizi na Raia wa Burundi, alitoa taarifa za uongo kwa ofisa wa uhamiaji.
Alidaiwa kuwa alijitambulisha kuwa ni raia wa
Tanzania na kuonesha Kitambulisho cha Taifa chenye jina lake ambacho alikipata
kinyume na sheria huku akijua kwamba anajiongezea kosa.
Kagoma alidai, Oktoba 19, 2013 katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wilayani Ilala Dar es Salaam, akiwa
mkimbizi na Raia wa Burundi, alishindwa kutimiza masharti yaliyotolewa Septemba
11, 2013 na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji ambapo alishindwa kurejesha hati ya
kusafiria aliyoipata isivyohalali.
Imeendelea kudaiwa kuwa, Juni 22, 2011 katika
Ofisi za Uhamiaji za Mkoa, alitoa taarifa za uongo katika fomu ya kuombea hati
ya kusafiria CT5 (Ai) yenye namba 05381440 kwa lengo la kupata hati hiyo.
Aidha mshtakiwa Bitaho anadaiwa kutoa taarifa
za uongo kwa kutoa kiapo kuonesha kuwa baba yake ni raia wa Tanzania kitu
ambacho sio kweli na kwamba alitoa barua kutoka Ofisi ya Kata ya Yombo Vituka
iliyomtambulisha kuwa ni Mtanzania kwa lengo la kupata hati ya kusafiria.
Mshitakiwa Bitaho alitoa pia barua ya kuajiriwa
aliyoambatanisha na fomu ya maombi ya hati ya kusafiria kuonesha ni Mtanzania
kitu ambacho alijua si kweli.
Aidha anadaiwa kujipatia kadi ya kupigia kura
kinyume na sheria na kwamba Mei 19 na pia amejihusisha na kazi kama Mwanasheria
Mkuu wa TBS bila kuwa na kibali.
No comments