HII NDIO KAZI CHADEMA WALIYOMPA MKE WA LOWASSA
Wanawake wa Chadema wamemtwishwa
Regina Lowassa mzigo wa kuongoza mapambano ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa
2020.
Akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu
la Wanawake wa Chadema (Bawacha) mjini Dodoma jana, Regina ambaye ni mke wa
waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa, alisema maandalizi ya uchaguzi huo
yanapaswa kuanza sasa.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,
Lowassa aligombea urais kupitia Chadema kwa kushirikiana na vyama vilivyounda
umoja wa katiba ya Wananchi (Ukawa) na hivyo kuweka ushindani mkubwa dhidi ya
chama tawala, ingawa hakushinda.
Jana, Regina alisema ushindi wa chama
hicho uko mikononi mwa wanawake wa Tanzania. “Kwanza niwashukuru sana kwa
mapambamo mliyoyafanya mwaka 2015. Nataka mfahamu kuwa bado Chadema inapendwa
na ina nguvu kubwa kuliko wakati mwingine. Msikatishwe tamaa bali tusonge
mbele,” alisema Regina.
Mama huyo aliwataka wajumbe kujiamini
zaidi na kupeleka ujumbe kwa wenzao ambao wamedhamiria kufanya mageuzi makubwa,
lakini akawataka wasilale.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee
aliwataka wanawake kujitoa zaidi katika kukisaidia chama hicho, hasa katika
maandalizi ya uchaguzi ujao.
Mdee aliwashauri wanawake wenye
nafasi, kama wabunge, kutumia nafasi zao kukisaidia chama.
Alisema wakati walionao kwa sasa si
wa kujivunia nafasi walizonazo, bali wanapaswa kuongeza nguvu zaidi na kugombea
nafasi za uongozi wa juu wa Chadema ili waendeleze mapambano ya ukombozi.
“Katika kipindi hiki ambacho tunaona
demokrasia inaminywa kwa vyama vyote vya siasa, ni vema wanawake ambao ni jeshi
kubwa tukawa mstari wa mbele katika mapambano si kurudi nyuma. Lazima kuwa na
nidhamu ndani na nje ya chama ili tufanikiwe katika vita hii,” alisema Mdee.
Katika kuonyesha msisitizo huo,
alimuagiza katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega kuwaandikia barua wabunge
ambao hawakuhudhuria kikao cha jana ili wajieleze kabla ya kuchukuliwa hatua.
Alisema ni jambo la aibu na fedheha
kwa viongozi kutoka mbali wakasafiri hadi Dodoma kwa ajili ya kikao, lakini
wabunge ambao wako mjini hapa wakashindwa kuhudhuria.
Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja
alisema chachu ya ushindi na mapambano ndani ya chama hicho kwa sasa ni kubwa
kwa kuwa wameamua kufanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya kuisaidia Chadema.
No comments