PROFESA MUHONGO KITANZINI TENA, RAIS MAGUFULI KUVIAGIZA VYOMBO VYA DOLA VIMUHOJI KWA KUSAINI MIKATABA MIBOVU YA MADINI
Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt
Magufuli ameagiza viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, Manaibu wake,
Wanasheria Wakuu wa Serikali, Makatibu Wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Maafisa wa TRA, na watumishi wengine waliohusika katika upotevu wa matrilioni
ya fedha kupitia sekta ya madini wahojiwe.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo
Ikulu alipokuwa akipokea ripoti ya pili ya kamati iliyokuwa ikichunguza
makinikia yaliyopo kwenye makontena bandarini iliyoundwa na wanasheria ya
wachumi.
Akizungumza kwa uchungu, Rais
Magufuli alisema kuwa Tanzania imejaliwa na kila aina ya madini ambayo unaweza
kuyataja hadi ukasahau lakini bado sisi ni maskini.
Akitaja baadhi ya madini alisema kuna
dhahabu, almasi, tanzanite, gesi za kila aina na vitu vingine mbalimbali lakini
tumebaki masikini kutokana na viongozi kutokuwa wazalendo.
Akisoma ripoti hiyo Ikulu leo,
Mwenyekiti wa Kamati, Prof. Nehemiah Osoro alisema kuwa Mawaziri wa Wizara ya
Nishati na Madini wa kipindi kilichopita walisaini mikataba ya madini ambayo
haikuwa na faida kwa taifa na hivyo kusababisha nchi kupoteza mapato kwa kutoa
misamaha ya tozo mbalimbali.
Prof. Osoro alieleza zaidi kuwa kwa
kutumia mamlaka aliyonayo, Mawaziri waliopita wamekuwa wakiwaongezea muda wa
kufanyakazi au eneo la uchimbaji makampuni ya madini bila kufuata sheria.
Akitolea mfano hapa, Prof. Osoro alisema kuwa, Waziri Prof.
Muhongo alifanya hivyo kwa mgodi wa North Mara.
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini
kipindi cha mwisho cha Rais Mkapa, Daniel Yona amewahi kushtakiwa kwa kosa la
kuongezea mkataba wa ukaguzi wa madini
kampuni MS ALEX STUWART kwa miaka miwili
zaidi kuanzia tarehe 14 Juni 2005 hadi tarehe
23 Juni 2007 bila kufuata utaratibu.
Rais ameagiza viongozi hao wahojiwe
ili waeleze kwanini walifanya waliyoyafanya na kwa manufaa ya nani kitu
kilichopelekea taifa kupoteza fedha nyingi.
Miongoni mwa watakaohojiwa kufuatua
amri hii ya Rais ni, William Ngeleja, Prof. Sospeter
Muhongo, Nazir Karamagi, Daniel Yona, Andrew Chenge, Fredrick Werema, Johnson
Mwanyika.
No comments