CUF LIPUMBA YATAMBULISHA BODI MPYA YA WADHAMINI.
Uongozi wa CUF, unaotambuliwa na
msajili wa vyama vya siasa nchini, umeitambulisha rasmi bodi mpya ya wadhamini
baada ya kupata usajili Juni 12, mwaka huu kutoka Wakala wa Ufilisi na Udhamini
(Rita).
Kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka
1992 ya vyama vya siasa, inakitaka kila chama cha siasa kilichosajiliwa kuwa na
bodi ya wadhamini iliyopata usajili Rita, ambayo itadumu kwa kipindi cha miaka
mitano.
Akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari leo, (Jumatano) Katibu Mkuu wa Bodi hiyo, Thomas Malima
amesema baada ya usajili huo, Baraza Kuu la Uongozi chini ya Mwenyekiti Profesa
Ibrahim Lipumba liliketi na kufanya uteuzi wa wajumbe tisa wa bodi hiyo baada
ya kujiridhisha bodi iliyokuwapo imemaliza muda wake.
“Sasa
chama kinarejea katika hali yake na kumaliza migogoro yote, baraza moja, kamati
ya utendaji moja na Bodi ya wadhamini moja, tunatoa onyo kali na tutamchukulia
hatua kali za kinidhamu mwanachama yeyote atakayesikika akitoa matamko yoyote
yanayohusiana na chama asiyetambuliwa kikatiba,” amesema Malima.
Kadhalika Malima ametaja maazimio ya
kikao cha bodi hiyo mpya kilichoketi Juni 17, mwaka huu na kusema bodi hiyo
iliadhimia kufuta kesi zote zilizofunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini.
Mengine yaliyoadhimiwa ni kuziandikia
benki zote zenye akaunti ya CUF zifungulie miamala yake na akaunti ya NMB tawi
la Temeke iwe akaunti ya bodi ya wadhamini.
No comments