RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI VIFO VYA WANANFUNZI 32

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya
wanafunzi 32 wa darasa la saba, walimu 2 na dereva wa gari la shule ya msingi
iitwayo Lucky Vicent ya Arusha vilivyotokea leo saa 3 asubuhi baada ya gari
walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu
Mkoani Arusha.
Wanafunzi na walimu hao walikuwa wakitoka shuleni kwao kwenda
shule ya msingi iitwayo Tumaini kwa ajili ya kufanya mtihani wa ujirani mwema
na walipofika katika eneo la Rhotia Marera basi walilopanda liliacha njia na
kisha kutumbukia korongoni ambako limesababisha vifo hivyo na majeruhi watatu.
Kufuatia ajali hii, Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za
rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo na kueleza kuwa ajali hiyo
imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia Taifa na imesababisha
uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na Taifa kwa
ujumla.
“Ndg Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo naomba
unifikishie pole nyingi kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi,
walimu na dereva waliopoteza maisha, hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, na
uwaambie naungana nao katika majonzi na maombi.
“Muhimu kwa sasa tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali
pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa
subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu” Amesema Mhe. Rais
Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Mei, 2017
No comments