MHE SAMIA: WAKANDARASI WAZALENDO KUPEWA KIPAUMBELE LAKINI KWA MIRADI ISIYOZIDI BIL 10

Serikali imeahidi kuendelea kuwapa kipaumbele
wakandarasi wazalendo katika utekelezaji wa miradi mikubwa lakini imewaonya
wale ambao wamekuwa wakitekeleza miradi chini ya viwango vilivyowekwa kwenye
mikataba.
Hayo
yalisemwa jana mjini Dodoma na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wakati
akifungua mkutano wa mwaka wa makandarasi ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa
Wakandarasi (CRB).
Samia
aliagiza kuwa miradi yote ya thamani isiyozidi Sh bilioni 10 wapewe wakandarasi
wa ndani hasa kwa miradi inayotekelezwa kwa fedha za ndani kwani wakandarasi
hao watasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania na kuongeza uwekezaji
ndani ya nchi.
Alisema
kuwapa miradi mikubwa wakandarasi wazalendo kuna faida kubwa kwani kutasaidia
kuwajengea uwezo hivyo kuweza kushindana na wakandarasi wa nje hivyo fedha
nyingi za serikali kubaki ndani.
“Tanzania
bora na yenye viwanda itatokana na wakandarasi bora na wenye uzalendo, hatuwezi
kufikia huko tunakotaka kwenda wakati miradi mikubwa ya ujenzi inafanywa na
wakandarasi wanje…. miradi ni yetu na fedha ni zetu hivyo lazima tuwape
nyinyi,” alisema.
Aidha,
aliwataka wakandarasi wazalendo wakamilishe kazi kwa wakati na kwa ubora
unaotakiwa pale wanapopewa miradi ili wajenge uaminifu kwa serikali kuendelea
kuwaamini na kuwapa miradi mikubwa.
Makamu
wa Rais aliwaonya baadhi ya wakandarasi wanaoshirikiana na maofisa wa serikali
kuongeza gharama kubwa za ujenzi wa miradi kwa misingi ya rushwa hali ambayo
imekuwa ikifuja fedha za serikali.
“Jamani
kwenye mkutano huu tujitathimini na tuanze upya maana kuna wenzetu ambao hawana
maadili na wanaendekeza rushwa, serikali ikitumia taasisi zake inatekeleza
miradi mikubwa kwa gharama ndogo lakini nyinyi wengine mnaweka gharama kubwa
ambazo si halisi,” alisisitiza.
Aliipongeza
CRB kwa namna inavyoendelea kuratibu kazi za wakandarasi wazawa huku akiitaka
kuendelea kuwajengea uwezo ili watekeleze miradi mikubwa kama kampuni ya nje.
“CRB
mmefanyakazi kubwa sana kuandaa mkutano huu na kwa kuwa mmekutana hapa naomba
mjadiliane kwa uwazi na muelezane ukweli kuhusu changamoto mlizonazo na namna
mtakavyozitatua na sisi serikali mkituletea maazimio yetu sisi tunaahidi
kuyafanyia kazi,” alisema.
Waziri
wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makame Mbarawa, yeye alisema asilimia 75 ya
madeni ya wakandarasi yameshalipwa na yaliyobaki yatalipwa wakati ukifika na
aliwaomba wawe wavumilivu wakati huu.
“Msidhani
serikali imewasahau, tunafanya kazi kwa bidii kuhakikisha wote mnalipwa kwa
sababu sisi tunaamini na tunafahamu kwamba ili makampuni yenu yaendelee lazima
mlipwe hela zenu hivyo endeleeni kuchapa kazi hela zilizobaki zinakuja,”
aliahidi Profesa Mbarawa.
Mwenyekiti
wa CRB, Consolata Ngimbwa, aliomba serikali iharakishe malipo ya wakandarasi
kwani wengi wao wako kwenye hali mbaya kifedha. Alisema baadhi ya wakandarasi
walifariki dunia kutokana kabla hatajalipwa malimbikizo ya madeni wanayoidai
serikali baada ya kukamilisha miradi mbalimbali ya ujenzi.
Alisema
wakandarasi wengi wazalendo wana uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi mikubwa ya
ujenzi hivyo aliiomba serikali iweke kipaumbele kwa kuwapa miradi hiyo.
Vile
vile, aliwageukia wakandarasi ambao wamekuwa na kawaida ya kutekeleza miradi
chini ya kiwango na wengine kutokomea mara baada ya kulipwa fedha za awali za
ujenzi.
Msajili
wa CRB, Rhoben Nkori aliwataka wakandarasi kutekeleza miradi wanayopewa na
kuahidi kuwa bodi yake itaendelea kuhakikisha mkandarasi asiye na viwango
anafutiwa usajili.
No comments