MHE JOHN HECHE AZIDIWA GHAFLA NA KUKIMBIZWA MUHIMBILI

Mbunge wa Tarime Vijijini kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche ameshindwa kuendelea kuhudhuria
vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini hapa, kutokana na matatizo ya kiafya na
kulazimika kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar
es Salaam.
Heche
alipata tatizo la afya na kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma jana alfajiri. Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk
Caroline Damian alikiri kuwa Heche, alipokewa hospitalini hapo alfajiri ya jana
na kuhudumiwa kwa muda kabla hajasafirishwa kupelekwa mahali ambako hakuwa
tayari kupataja.
“Hatujampa
rufaa ila matibabu yake yanaratibiwa na Kliniki ya Bunge, hivyo tulimpokea na
kumhudumia kwa muda kabla taratibu za kumsafirisha hazijakamilika, tulipoambiwa
ndege ya kumsafirisha ipo tayari, aliondolewa kwetu na kusafirishwa kwa ajili
ya matibabu,” alieleza daktari huyo.
Awali,
mbunge huyo alipata tatizo la afya na kulazimika kuwa chini ya uangalizi wa
kitabibu. Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu,
alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akijibu maswali ya wananchi
walihoji hali ya mbunge huyo, ambaye ilikuwa ikielezwa kuwa hospitalini.
Kabla
ya muda huo kuwadia, ilielezwa kuwa Heche alipata maumivu ya tumbo kabla
hajapelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili ambako alifanyiwa
upasuaji.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema Taifa, Tumaini
Makene jana alithibitisha taarifa ya
kuugua ghafla kwa Heche na kuletwa jijini Dar es Salaam katika hospitali hiyo.
“Ni
kweli Heche aliugua ghafla akiwa Bungeni huko Dodoma, alisafirishwa kwa ndege
jana asubuhi saa moja na kuletwa Muhimbili ambako anaendelea na matibabu,”
alisema Makene.
Ofisa
Habari wa Muhimbili, Neema Mwangomo alithibitisha kupokelewa Heche jana saa nne
asubuhi na kwamba anaendelea na vipimo kubaini nini tatizo lake.
No comments