Waziri Wa Afya Ataja Vipimo Na Dawa Za Malaria Zinazotakiwa Kutolewa Bure
Serikali
ya Tanzania imepiga marufuku vituo vya Umma kuwalipisha wananchi wanaokwenda
kupima maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa kipimo cha MRDT na utoaji wa dawa
za mseto (ALUU) zinazotumika kutibu ugonjwa huo kuanzia sasa.
Akizungumza
na waandishi wa habari wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Malaria
duniani mjini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Bi. Ummy Mwalimu amesema vipimo hivyo ni bure na pia mgonjwa asilipishwe
fedha kwa dawa za mseto.
“Napenda
kusisitiza vituo vya umma vinavyotumia vipimo vya MRDT kwa wagonjwa wa malaria,
vipimo hivyo ni bure na pia mgonjwa asilipishwe fedha kwa dawa za mseto ama
yule anayelazwa kuchomwa sindano ya ugonjwa huo….Waganga wakuu wa mikoa na
wilaya, hakikisheni kuanzia sasa mnafuatilia wahudumu wote na watakaokiuka
agizo hili watachukuliwa hatua za kisheria mara moja”. Alisema Bi. Ummy
Aidha,
Bi. Ummy amewataka wananchi kushirikiana na serikali kuwafichua wahudumu wa
Afya ambao watawalipisha fedha pindi watakapo kuwa wanapima huduma ya Malaria
kupitia kipimo cha MRDT ama watakapohitajika kupewa dawa ya mseto (ALUU), pia
amezionya maabara binafsi ambazo
zimekuwa zikifanya kazi zake kwa kuangalia zaidi fedha badala ya maisha
ya mtu kama kuwaambia wana maambukizi ya malaria wakati hawana.
Pamoja
na hayo, amesema takwimu kutoka katika vituo vinavyotolea huduma za afya
zinaonyesha takribani watu milioni 12 wanaugua ugonjwa huo kwa mwaka ambapo
katika tafiti hizo mkoa wa Kagera, Geita na Kigoma ziliweza kuonekana na
viwango vikubwa vya maambukizo kwa mwaka 2015 na 2016 huku wajawazito na watoto
chini ya miaka mitano kuonekana kuathiriwa zaidi.
No comments