RAIS MAGUFULI KUFUNGUA KONGAMANO LA MAADILI
RAIS Dk. John
Magufuli anatarajiwa kufungua kongamano la maadili lililoandaliwa na
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Akizungumza kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu
Aboubakar Zuberi Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis
Mataka, alisema kongamano hilo litafanyika Aprili 24.
Alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili mmomonyoko wa
maadili uliopo ndani ya jamii hivi sasa.
“Kongamano hili limeandaliwa na
Bakwata ambapo litahudhuriwa na masheikh mbalimbali pamoja na viongozi wa
kidini kutoka mikoa mbalimbali, lengo likiwa ni kuangalia jinsi maadili
yalivyoporomoka na kutafuta mbinu ya kuijenga jamii iliyo bora,” alisema Sheikh Mataka.
Alisema kongamano hilo la siku moja litafungwa na Rais wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Alisema wengine watakaohudhuria kongamano hilo ni wajumbe wa
Ulamaa Taifa, masheikh kutoka taasisi mbalimbali, viongozi wa kidini kanda,
mabalozi, wakuu wa vyombo vya usalama na wananchi walioalikwa.
Sheikh Mataka alisisitiza kuwa maadili ni muhimu ndani ya jamii
na kwamba kwa sasa nchi inakabiliwa na mmomonyoko wa maadili.
“Ukiona jamii inazungukwa na walevi,
watumiaji dawa za kulevya, binadamu wengine wanafurahia wenzao wakiuawa au
kupata ajali, ni hali ya kupoteza mwelekeo wa maadili,” alisema Sheikh Mataka.
No comments