HOJA YA KUTAJA WABUNGE 11 WATAKAOTEKWA YAZIMWA, SALAMA WA TAIFA WAPIGWA MARUFUKU BUNGENI
Mazoea ya baadhi ya wabunge kuomba mwongozo wa kiti cha spika
kuzima hoja za wabunge wenzao, jana uliibuka tena baada ya Mbunge wa Makambako,
Deo Sanga kuomba mwongozo uliozima hoja ya kutaja majina ya wabunge 11 wanaodaiwa
kutaka kutekwa.
Sanga aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni 68 (7) pamoja
na 64 A,B,C, alisema ndani ya Bunge yameongelewa mambo yanayohusu mahakama,
usalama, mauaji na kutekwa.
“Nilikuwa nadhani kupitia kanuni hizi
naomba mwongozo wako nini kazi ya Bunge mheshimiwa naibu spika,” alisema.
Mwongozo huo uliibuka baada ya Mbunge wa Viti Maalum CCM,
Angelina Malembeka kuwataka wabunge waliosema kuna orodha ya wabunge 11
wanaotakiwa kutekwa kuwataja majina yao.
Hoja ya Malembeka ilimlenga Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein
Bashe ambaye siku za karibuni aliliambia Bunge kwamba ameambiwa na mmoja wa
mawaziri kuwa kuna wabunge 11 watatekwa na Usalama wa Taifa.
Malembeka alitoa hoja hiyo wakati akichangia mjadala wa hotuba
ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Tamisemi na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Hata hivyo, mwongozo wa spika ulioombwa na Sanga ulizima kiu ya
Malembeka aliyetaka kumbana Bashe ataje majina ya wabunge hao 11, badala ya
kutaja idadi pekee.
Akijibu mwongozo wa Sanga, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson
aliamua kupiga marufuku masuala ya Usalama wa Taifa kujadiliwa bungeni.
Dk Tulia alisema wanaotaka kufanya hivyo wawasilishe hoja
mahsusi kwa kufuata Kanuni za Kudumu za Bunge.
Awali, Malembeka alisema ni vizuri Usalama wa Taifa wakaongezwa
fedha, mbinu mpya na vifaa ili kurahisisha utendaji wao wa kazi.
“Kutwa mtu anatuma ujumbe kwenye simu
kwa rafiki yake eti nimetekwa nyara, waulizeni waliotekwa hiyo simu wamepata
wapi ya kutumia huo ujumbe kuwa wametekwa?
“Kutekwa nyara si mchezo, waulizeni
wenzenu waliotekwa
watawaambia si mchezo. Na hao
wanaojifanya usalama feki naomba mheshimiwa waziri uwashughulikie kwa sababu
sasa mtu akishakata ‘panki’ lake akavaa kaunda suti yake anatoa kitambulisho
anasema mimi Usalama wa Taifa.
“Usalama wa Taifa mchezo! Mtu
anajizungusha zungusha
anawatisha watu mtaani unasema
Usalama wa Taifa sasa wale wanaojifanya Usalama wa Taifa na kuogopesha watu
mtaani washughulikiwe,” alisema.
No comments