MAMBO MANNE YANAYOATHIRI MALEZI YA MTOTO
KATIKA malezi ya mtoto ya kila siku zipo changamoto ambazo
zinachangia kumjenga katika makuzi na nyingine zinaweza zikamuharibu.
Changamoto zote hizi zinapaswa kutatuliwa ili mtoto aweze kukua
katika utaratibu mzuri unaoleweka.
Makuzi ya mtoto/watoto ni jukumu la muhimu sana kwa mzazi yo yote
katika jamii.Katika tafiti mbalimbali za kisayansi makuzi anayopata mtoto
kuanzia umri wa miaka sifuri hadi 12 yanaakisi tabia atakayokuwa nayo katika
utu uzima wake.
Kutokana na hali hiyo kuna mambo manne ambayo mzazi unapaswa
kuyaangalia ili kuepuka kuathiri makuzi ya mtoto.
Moja ni kumuaibisha,hatua za kinidhamu unazochukua dhidi ya mtoto
wako huathiri malezi yake.
Wataalam wa malezi ya watoto wanashauri malezi yetu yawe
shirikishi kwa maana ya kwamba kila unapomkataza mtoto kufanya jambo fulani
kama vile kutukana watu, utoro shuleni, ugomvi n.k ni vizuri zaidi ukawa
unamfahamisha ni kwa nini haifai kufanya jambo fulani.
Lengo ni kumpatia nafasi ya kuhoji/kutafakari/kuelewa badala ya
kumshurutisha tu kutekeleza maagizo.
Kwa kufanya hivyo, unampa uwezo wa kupambanua, kuelewa na
kujiamini katika maamuzi mbalimbali. Pia hatua kali za kinidhamu kama vile
kumchapa mtoto zinaweza kusababisha hofu kwa watoto wako, ambayo huathiri uwezo
wao wa kuwasiliana na wewe, walimu na wezake.
Hata hivyo, pia haitakiwi kuwa mpole mno kwa sababu watoto
wanaweza kuendelea kwa wakosefu wa nidhamu na kuathiri mwenendo wao katika
jamii na shuleni.
Jambo la pili ni mazingira,neno mazingira kwa tafsiri fupi ni vitu
vyote vinavyotuzunguka hewa, miti, majengo, watu, wanyama, shule, nyumba za
ibada .n.k.
Mazingira ya mtoto yanaathiri ya moja kwa moja kwa mtoto hasa ya
nyumbani na shuleni. Muda mwingi wa makuzi ya watoto hutumika nyumbani na
shuleni.
Mtoto anayetoka kwenye nyumba ambayo wazazi wake wako katika hali
ya ugomvi kila mara, umasikini, utajiri n.k. mambo hayo umuathiri moja kwa moja
kimtazamo wa kimaisha.
Jambo la tatu la kuangalia ni mawasiliano,mtoto anapaswa
kushirikishwa katika baadhi ya maamuzi ya kifamilia kama vile masuala ya
chakula, vinywaji, maongezi n.k.
Ninaposema kushirikishwa katika suala ya chakula ni katika hali ya
kujenga tabia ya ushirikishwaji na kumpa uhuru wa maamuzi kumuuliza mtoto leo
unataka kula nini mama/baba ni kuonyesha kuthamini mawazo yake.
Pia katika maongezi nina maana mtoto akisema jambo lolote ni
muhimu kumsikiliza na siyo vizuri kumpuuza au kumkaripia kwamba anapiga kelele.
Tabia hiyo, itamsaidia kwa kumpatie uwezo wa kujieleza na
kujisikia kuthaminiwa na wazazi wake.
Mbali na hayo mfumo wa malezi pia unaweza kumjenga mtoto wako au
kumuharibu.
Kuweka ratiba ya kukaa na watoto na kuongea nao na kusikiliza
mawazo hayo huwajengea hali ya kujisikia kuathaminiwa na kupendwa na
wazazi/walezi na hivyo kuwaongezea furaha na amani
Pia tabia hii huwajengea hali ya kujiamini na uhuru wa kueleza
hisia zao nyumbani na shuleni bila hofu kwa sababu ya Imani ya kupendwa
imejengwe kwenye akili zao.
Wazazi tuna jukumu kubwa katika kujenga watoto wetu kisaikologia
katika akiwa mdogo,kumjenga ukubwani ni vigumu kwakuwa akili inakuwa
imeshakomaa.
NA AZIZA MASOUD-MTANZANIA
No comments