KAMANDA SIRO: WALIOFANYA VURUGU MKUTANO WA CUF WAMEKAMATWA
Saa tatu baada ya viongozi wa CUF kukutana na
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuhoji sababu
za kutokamatwa watu waliofanya vurugu kwenye mkutano wa waandishi wa habari na
viongozi wa chama hicho wa wilaya ya Kinondoni, Jeshi la Polisi limetangaza
kushikilia watu watatu.
Wakiongozwa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho Julius Mtatiro, viongozi hao
waliwaeleza wanahabari kuwa ni ajabu kuona
Polisi haijachukua hatua huku ikijulikana wazi kuwa watu hao walijeruhi
wanahabari na viongozi wa chama hicho katika tukio ambalo liliripotiwa na
vyombo vya habari.
Viongozi
hao walikutana na Sirro jana saa 5 asubuhi na kuzungumza kwa takribani saa
moja, na kisha saa 8 mchana Kamanda huyo alizungumza na waandishi wa habari na
kueleza kukamatwa kwa watu hao, wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo.
Jumamosi
iliyopita takribani watu watano wakiwa kwenye gari lenye nembo na bendera za
CUF, walivamia mkutano huo uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli ya Vinna, Mabibo
wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.
Miongoni
mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso kininja alichomoa bastola na
kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na wenzake, jambo
lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia kipigo.
Katika
ufafanuzi wake, Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande unaomwunga
mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad lakini vyombo vya
Dola viko kimya.
“Baada
ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa kimya ili kuona kama polisi watasema
chochote ila imekuwa tofauti. Wako kimya tu,” alisema Mtatiro.
Akieleza
kilichowapeleka kituoni hapo, alisema: “Tulitaka kujua yule mvamizi aliyekuwa
na bastola mpaka sasa yuko wapi. Mvamizi mmoja tunajua alikamatwa na wananchi,
akapigwa kidogo na kuokolewa. Tulitaka kujua alitoa maelezo gani.”
Alisema
baada ya tukio hilo, Mkuu wa Upelelezi aliwapigia simu viongozi waliovamiwa
akiomba waende kituo cha Polisi Magomeni
wakapatanishwe.
“Tulishangazwa
na taarifa hiyo, kwa watu waliovamiwa kwenda kupatanishwa. Tulijihoji kama
Jeshi la Polisi linaweza kupatanisha watu wenye makosa ya jinai, kwani mtu wa
makosa hayo upelelezi unapokamilika hupelekwa mahakamani,” alisema Mtatiro.
Alisema
sababu nyingine ya kwenda kituoni hapo ni kutaka kufahamu kama watu wanaofanya
matukio hayo wako juu ya sheria.
“Tulimwonya
Kamanda Sirro kwamba sisi (upande wa Maalim) tuna nguvu kuliko Lipumba na
kuiomba Polisi kutekeleza majukumu yake kwa kuchukua hatua dhidi ya wavamizi
hao,” alisema.
Katika
mkutano wake na wanahabari, Sirro alisema Polisi inashikilia watu watatu
wakituhumiwa kufanya vurugu kwenye mkutano huo.
“Tulipata
taarifa ya kuvamiwa kwa mkutano wa wanachama wa CUF na watu wasiofahamika
wakiwa na silaha. Baada ya taarifa hizo kupokewa askari walifuatilia na
kukamata watu watatu,” alisema Sirro.
Alisema
watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria
zitafuatwa.
Alisema
hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa waliohusika watasakwa kokote
watakokuwa.
No comments