RAIS MAGUFULI: VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA SIYO YA MZAHA WALA KUANGALIA MAJINA YA WATU, VYEO VYAO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameviagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha vinasimamia sheria ipasavyo ili kukabiliana na tatizo hilo hapa nchini.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 12 Februari, 2017 Ikulu Jijini Dar
es Salaam, muda mfupi baada ya kuwaapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers William Siyanga, Kamishna Jenerali wa
Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe.
Joseph Edward Sokoine, Balozi wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Omar Yusuf Mzee
na Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Grace Aaron Mgovano.
Mhe.
Dkt. Magufuli amewataka viongozi wote wa Serikali kuungana na vyombo vya dola
katika mapambano dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za
kulevya na ametaka mapambano hayo yasifanywe kwa mzaha wala kwa kuangalia
majina ya watu, vyeo vyao na taasisi wanazoongoza.
Mhe.
Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote wa mikoa walioanza kukamata watu
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na amewaomba Watanzania wote
waunge mkono juhudi za kukabiliana na wanaofanya biashara na kutumia dawa za
kulevya ambazo zinazidi kuangamiza nguvukazi ya Taifa.
“Niwaombe
ndugu zangu tuungane katika vita hii dhidi ya dawa za kulevya, waandishi wa
habari na wana mitandao tuweke mbele Utanzania wetu, akitokea mtu anapambana na
dawa za kulevya tumuunge mkono badala ya kumchafua.
“Vita
hii ni kubwa hatuwezi kwenda nayo kwa mzaha na Serikali itahakikisha inasimamia
sheria namba 5 ya mwaka 2015 iliyohusu kuzuia na kupambana na dawa za kulevya
ambayo ilitungwa na Bunge la 10 lililoongozwa na Spika Anna Makinda na sheria
hiyo ikatiwa saini na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, nawapongeza sana kwa kutunga sheria hii.” Amesisitiza Mhe. Rais
Magufuli
Pia,
Mhe. Dkt. Magufuli amesema takwimu zinaonesha kuna watanzania 1,007 wamekamatwa
na kufungwa gerezani katika nchi mbalimbali baada ya kupatikana na makosa ya
kujihusisha na dawa za kulevya, na amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika
nchi hizo kutojihusisha kuwatetea waliofungwa kwa makosa hayo na badala yake
waache sheria za nchi husika zichukue mkondo wake.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna
Peter Makakala kufanya mabadiliko makubwa ndani ya Idara ya Uhamiaji nchini
kutokana na utendaji wake kutoridhisha.
“Nataka
ukafanye mabadiliko makubwa (Total Reform), nataka Uhamiaji izalishe fedha kwa
ajili ya nchi hii, nataka ukadhibiti utoaji hati za kusafiria (Passports) maana
zimekuwa zikitolewa hovyohovyo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Hafla
ya kuapishwa kwa viongozi hao pamoja na kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa
umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela,
imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe.
Kassim Majaliwa, Kaimu Jaji Mkuu Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Mawaziri, Makatibu
Wakuu wa Wizara mbalimbali na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
12
Februari, 2017
No comments