Breaking News

MKE WA BILIONEA MSUYA AACHIWA HURU NA KUKAMATWA TENA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mwenzake Revocatus Muyela wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya Aneth Msuya.

Hata hivyo washtakiwa hao walikamatwa tena na jeshi la polisi.

Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa leo amewaachia huru washtakiwa hao baada ya upande wa mashtaka kushindwa kutimiza amri yake iliyowataka kufanyia marekebisho ya hati ya mashtaka

Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia.

Uamuzi wa mahakama kuifuta kesi hiyo umefikiwa leo baada ya jalada la kesi hiyo lililokuwa limeitwa Mahakama Kuu kurejeshwa mahakamani hapo.

Februari 20, mwaka huu, Hakimu Mwambapa aliupatia upande wa mashtaka muda wa siku tatu kurekebisha hati ya mashtaka.

Lakini mpaka siku hizo tatu zinaisha hawakuwa wamefanyia bali  Wakili wa Serikali, Hellen Moshi aliiambia mahakama kuwa baada ya ofisi yao kutafakari kwa kina wameamua kuwa hawana cha kubadilisha kwa hati hiyo ya mashtaka

Wakili wa utetezi,  Peter Kibatala alidai kuwa upande wa mashtaka licha ya kupewa muda wa kutosha kufanyia marekebisho hati hiyo lakini wamekaidi amri hiyo.

Kibatala aliiomba mahakama kuwaachia washtakiwa huru kwa kuwa amri ya mwisho ya mahakama ilisema kama wasipofanya marekebisho itachukua hatua  na pia hakuna rufaa yoyote iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupinga uamuzi huo.

Hakimu Mwambapa amesema,kweli mahakama imeamuru upande wa mashtaka kufanyia marekebisho hati ya mashtaka pindi ilipoona inamapungufu lakini hawakufanya hivyo, akawaongezea muda hawakufanya hivyo, Ila leo wamekuja na maelezo ya kuwa hati ya mashtaka ni sahihi.

"Hati ipi ambayo ipo sahihi wakati mahakama ilisema haipo sahihi, nawaachia huru washtakiwa", amesema Mwambapa.

Awali ndugu wa marehemu waliwasilisha barua mahakamani hapo na Kwa mujibu wa barua hiyo walikuwa wanataka Hakimu huyo ajitoe kwa sababu hawana imani naye.

Hakimu Mwambapa alikuwa atoe uamuzi juu ya hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi pamoja na upande wa mashtaka ambapo Wakili John Malya aliomba washtakiwa hao waachiwe huru kwa sababu   hakuna hati ya mashtaka inayowashikilia washtakiwa hao mahakamani hapo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa yeye aliiomba mahakama iwape muda ili waweze kutekeleza amri ya mahakama iliyotolewa Januari 9, mwaka huu

Washtakiwa Miriam na Revocutus  wanadaiwa kumuua kwa makusudi Aneth Msuya, kwa kumchinja, nyumbani kwake Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Miriam  ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo alikuwa mke wa aliyekuwa kaka wa Aneth, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama bilionea Msuya.

Erasto Msuya, ambaye alikuwa mfanyabiashara bilionea wa madini ya Tanzanite, pia aliuawa kwa kupigwa risasi, Agosti, 2015 eneo la Mijohoroni,  kando ya barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo washtakiwa hao walikamatwa tena na kuondoka na gari la polisi.

No comments