WAZIRI MKUU; MWANAFUNZI AKIPATA MIMBA MZAZI JELA MIAKA 30
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa wazazi wote wawili wa mtoto wa kike atakayekatishwa masomo na kulazimishwa kuolewa ama akipata ujauzito.
Aidha
amesema Serikali itamfunga jela miaka 30 kijana anayetaka kumuoa msichana
anayesoma pamoja na wazazi wake.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kumlinda mtoto wa kike katika kuhakikisha
kuwa anapata haki yake ya msingi ya kusoma kufikia elimu ya chuo kikuu kwa
kujenga mabweni na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaowapa mimba
na kuwaozesha katika umri mdogo na kukatisha masomo yao.
Majaliwa
aliyasema hayo jana wilayani Hanang, mkoani Manyara katika ziara yake ya kikazi
ya siku sita kwa mkoa huo.
Alisisitiza
kuwa kupitia sera ya kuboresha elimu nchini serikali imeondoa michango ya fedha
za kulipia bili za maji, umeme, gharama za mlinzi na mitihani ili kumpunguzia
gharama mzazi na mlezi na kuwaacha wazazi kushughulikia maeneo mengine muhimu
kwa mtoto wao.
Alisema
tayari kwa mwaka huu wa fedha, walimu 4,396 wa masomo ya sayansi wameajiriwa
ambapo alisisitiza kuwa wazazi na walezi wanalo jukumu kubwa la kusimamia
maendeleo ya shule ya watoto wao kwa lengo la kupandisha ufaulu wa elimu kwa
wilaya,mkoa na taifa.
“Mtoto
akiwa mtoro baba na mama wa mtoto huyo atashitakiwa,mtoto wa kike
asiguswe,vijana waendesha bodaboda acheni kuwalaghai watoto hao kwa zawadi na
usafiri, tutawasaka wote,” alisisitiza.
Akizungumza
na watumishi wa umma katika halmashauri ya wilaya hiyo, aliwataka watumishi hao
kujivunia serikali yao kwa kuienzi katika kufanya kazi kwa nidhamu katika
kuwatumikia wananchi bila kujali uwezo wao, kabila wala rangi zao kwa kuwa
wamepewa dhamana ya kusikiliza kero zao.
Majaliwa
alifafanua kuwa wafanyakazi wana wajibu wa kuwatumikia watanzania kwa kuwa wao
ni waajiriwa wa serikali hivyo ni muhimu wakatoka maofisini na kwenda vijijini
kusikiliza kero na kuzitatua badala ya wananchi kungojea viongozi wa kitaifa
kuja kusikiliza kero na malalamiko yao wakati wao ni watendaji wakuu katika
maeneo yao.
“Utumishi
wenu hauhitaji upendeleo ama ahadi za njoo kesho, utumishi wa awamu ya tano ni
wa uwajibikaji zaidi na uwajibikaji ni pamoja na kuwa mwaminifu katika kulinda
na kusimamia kikamilifu fedha za serikali zinazotengwa katika halmashauri
husika kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
Akizungumzia
soko la kimataifa la Endagaw, aliwapongeza wananchi wa wilaya hiyo kwa
kukubaliwa kujengewa soko kubwa la kimataifa ambako wakulima watapeleka mazao
yao na kuyauza lakini pia wataweza kuingiza mapato kwa kukodisha makampuni
makubwa yanayohitaji kukodi kuhifadhi mazao kama NRFA.
Aliwataka
wakulima wa mazao mbalimbali wilayani Kateshi kulitumia soko la mazao la
kimataifa la Endagaw lililojengwa na ofisi yake kuuza mazao yao kwa bei nzuri
badala ya kuuza mazao majumbani ambako wamekuwa wakiuza kwa bei ya chini
isiyowasaidia kukuza kipato chao.
Alieleza
kuwa serikali itaendelea kjuimarisha miundombinu ya soko hilo kwa kujenga eneo
la wazi la nje kudhibiti magari makubwa yanayoshusha na kupakia mizigo
yasikwame kutokana na matope na kuwa na mizani ya kupimia mazao na magari.
Kuhusu
kero ya maji katika mji wa Katesh, alisema marekebisho yanafanyika kurekebisha
mashine ya kuvuta maji na kuhakikisha sera ya maji inatekelezwa kwa vitendo
katika kumpatia maji kila mwananchi umbali usiozidi mita 400.
Awali
katika taarifa yake Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Sara Msafiri alimweleza Waziri
Mkuu kuwa changamoto kubwa inayoikabili wilaya hiyo ni migogoro ya ardhi,
kuanzisha gereza la wilaya kupunguza usumbufu wa kuwapeleka wahalifu Babati,
jambo ambalo alisema atalipeleka wizara ya mambo ya ndani lipate kushughulikiwa.
Msafiri
aliomba pia kujengewa mahakama ya wilaya ambapo alisema ni mchakato uliopo wa
mahakama kuu kujenga mahakama katika ngazi za wilaya hivyo jambo hilo nalo
litashughulikiwa.
Mbunge
wa Viti Maalum Mkoa, Ester Mahawe alibainisha tatizo la kuwa na shule ya kidato
cha tano na sita moja kwa wilaya nzima ambapo alimwomba Waziri Mkuu kutoa
kipaumbele katika bajeti zake za elimu ili shule zaidi zijengwe mkoani humo.
Mbunge
wa Viti Maalumu Mkoa wa Manyara, Rose Kamili (Chadema) aliiomba serikali kufuatilia
na kuyatolea maamuzi mashamba makubwa ambayo yamekuwa hayaendelezwi na
wawekezaji kutoka Ngano Ltd wanayoyamiliki zaidi ya ekari elfu 45 ambapo
wamekuwa wakilima ekari elfu 16 pekee na kuacha migogoro ya ardhi baina yao na
wananchi na kukosesha mapato ya halmashauri.
Ziara
hiyo ilipata baraka za mvua kubwa baada ya ukame wa muda mrefu ilishangiliwa na
umati wa watu waliokuwa wakiimba kwa furaha kuashiria Waziri Mkuu kuja na
baraka hiyo kuneemesha mazao yao.
Leo
Waziri Mkuu anatarajiwa kuhitimisha ziara yake wilayani Babati ambapo pamoja na
mambo mengine atafanya majumuisho ya ziara hiyo na kutoa maelekezo ya serikali
kwa wananchi na viongozi ngazi ya mkoa.
No comments