KAMATI NDOGO YA KAMATI KUU YA CHADEMA YABARIKI MBOWE AMSHITAKI MAKONDA KWA KUMDHALILISHA
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimejipanga na kitampatia
mawakili wa chama Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe katika hatua yake ya
kumfungulia kesi ya kikatiba na ya madai Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda.
Februari
8 mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitaja majina 65 kwa
tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya akiwamo Mbowe na kuwataka
kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.
Lakini
siku moja baadaye Mbowe aliitisha mkutano na waandishi wa habari akiwa mjini
Dodoma ambapo alieleza kutofika polisi kwa wito wa Makonda akisema hana mamlaka
hiyo isipokuwa pale tu taratibu za kisheria zitakapofuatwa.
Mbowe
ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni aliweka bayana nia yake ya
kumfungulia mashtaka ya madai Makonda kwa kumkashifu na kumchafulia jina.
Akitoa
maazimio ya kikao cha kamati ndogo ya Kamati Kuu ya Chadema jijini Dar es
Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Abdalah Safari alisema
kamati hiyo inaunga mkono hatua ya Mbowe kumfungulia kesi ya kikatiba Makonda.
“Katika
hili tumejipanga kweli kweli…tutaungana na Mbowe katika kesi hii na tutampatia
mawakili wa chama akiwamo mimi na tuko wengi,”alisema.
Profesa
Safari aliwataka wote ambao walitajwa na wanaamini kuwa walionewa kujihusisha
na biashara au utumiaji wa dawa za kulevya wafungue mashauri mahakamani.
“Tunatoa wito kwa wale wengine wote ambao
walitajwa na wanaamini kuwa walionewa, kuchafuliwa majina na au kudhalilishwa
wafungue mashauri mahakamani, kwani hii ndio njia pekee ya kuzuia wengine
wasifanyiwe uonevu kama huu siku zijazo,”alisema Profesa Safari.
Pamoja
na mambo mengine, Profesa Safari alisema tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu
2015 viongozi na wanachama wa Chadema wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa kwa
makosa ya kubambikiziwa kwa kisingizio cha uchochezi.
Alisema
mpaka sasa jumla ya wanachama na viongozi 215 wamefunguliwa kesi zaidi ya 78
nchi nzima.
“Kati
ya hao wengi wao wamenyimwa dhamana bila sababu za msingi huku wale ambao
walipatikana na hatia walipewa adhabu za vifungo bila kupewa fursa ya faini.
“Kutokana
na hilo, hivi sasa tunaandaa orodha kamili itakayoainisha kesi zote za jinai
ambazo ziko mahakamani na kuonyesha aina ya mashtaka na vifungo vilivyotolewa
ambayo itawekwa wazi kwa vyombo vya habari na taasisi za ndani na nje ya nchi
kuthibitisha kuwa kuna mpango wa kuwafunga viongozi wa upinzani kwa kusudi ili
kuwadhoofisha,”alisema Profesa Safari.
Katika
hatua nyingine Profesa Safari aliwaomba marais wastaafu, mawaziri wakuu
wastaafu na majaji wastaafu kuzungumza na Rais John Magufuli kutokana na
yanayoendelea na kwamba wasiogope kwani wao hawatatumbuliwa.
“Marais wastaafu Ali Hassani Mwinyi, Benjamin
Mkapa na Jakaya Kikwete wanaogopa nini? Kwanini wasimwambie Rais Magufuli kuwa
na wao waliapa kuilinda Katiba ya nchi hivyo na yeye afanye hivyo.
“Mawaziri
wakuu wako wapi? Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba, Dk. Salim Ahmed Salim huyu
amekuwa kimya kabisa na alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Majaji
wastaafu nao wako kimya. Tunaomba waache uoga wajitokeze wao
hawatatumbuliwa,”alisema Profesa Safari.
No comments