WAZIRI MKUU: MARUFUKU KUUZWA POMBE ZA VIROBA HAPA NCHINI KUANZIA MARCH 1
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema kuanzia Machi mosi, 2017 Serikali itapiga marufuku matumizi ya pakiti
za plastiki kufungashiwa pombe kali maarufu kwa jina la ‘viroba’.
“Tumekaa na wenye viwanda na
kukubaliana kuwa wanaotengeneza Pombe waziweke katika ukubwa unaokubalika.
“Sasa hivi viroba vimeenea kila kona hata watoto wa shule za msingi wanatumia
kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo. Kuanzia tarehe moja
Machi, tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye.”
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Alhamisi, Februari 16, 2017) wakati akizumgumza na maelfu ya wakazi wa mji
mdogo wa Mererani, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake
mkoani Manyara.
Amesema agizo hilo linaenda
sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya kwani mji wa Mererani unaongoza kwa
matumizi ya dawa hizo haramu.
“Tutawakamata wanaosambaza,
wanaouza na wanaokula. Hapa Mererani kuna bangi, kuna mirungi, cocaine na
heroine. Mkuu wa Mkoa hapa panahitaji operesheni kupambana na dawa za kulevya.
Piteni kwenye vijiwe na kukagua wale waliolegealegea, kisha tuwapime,”
alisisitiza.
Akifafanua suala la uwekezaji
kwenye eneo la Shambalai kutokana na ujumbe ulioandikwa kwenye mabango, Waziri
Mkuu alisema katika eneo hilo zimetengwa ekari 500 kwa ajili ya EPZA ili kujenga
miundombinu mbalimbali.
“Hilo eneo ni la uwekezaji kwa
ajili ya ujenzi wa viwanda, masoko na maduka makubwa (malls). Sote tunafahamu
kuwa Tanzania hivi sasa inaweka msisitizo juu ya ujenzi wa viwanda. Pale
tunataka tuwe na viwanda vya nyama, vya kushona nguo na kuchakata madini ya
Tanzanite ili kjongeza thamani,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema kama kuna mtu ana
uhakika kuwa nyumba yake bado haijalipwa fidia katika eneo lile, aende akaonane
na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Joel Bendera lakini taarifa alizopewa ni kwamba hakuna
mtu ambaye hajalipwa.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewaita wakurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One ili wampatie taarifa juu
ya malalamiko yanayotolewa na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwamba hali ilikuwa
nafuu wakati kampuni hiyo ikimilikiwa na wazungu kuliko hivi sasa.
“Nikimaliza ziara ya mkoa huu,
nataka tarehe 27 Februari, Wakuu wa hii kampuni waje ofisini kwangu na taarifa
kuhusu shughuli za uendeshaji wa madini. Nitawashirikisha na wabunge wenu ili
waje waseme kwa nini mzungu ni bora kuliko Mtanzania,” alisema.
“Serikali hii inatarajia kuona
Watanzania wakinufaika na rasilmali zao. Haiwezekani tukahimiza uwekezaji wa
ndani halafu leo anasifiwa mzungu kuliko mzawa,” alisema.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA,
FEBRUARI 17, 2017.
No comments