TANZANIA KUJIFUNZA KWA CHINA KUHUSU NAMNA YA KUKUZA UCHUMI
Serikali imesema iko tayari kujifunza namna
ambavyo China imefanikiwa katika kukuza uchumi wake, ili kutengeza mfumo
utakaoleta maisha bora kwa Watanzania wote.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan wakati akifungua sherehe za Mwaka Mpya wa China, ambao kwa mwaka
huu unajulikjana kama ‘Mwaka wa Jogoo” katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es
Salaam.
Samia alisema mafanikio ya China katika
kuwatoa wananchi wake katika umasikini, unaendelea kuihamasisha Serikali na
hasa katika kipindi hiki ambacho inaongia katika mageuzi ya kiuchumi.
“Tunaridhishwa jitihada zenu katika
kumaliza tatizo la rushwa, tunafahamu mabadiliko mliyofanya ndio yametoa
matokeo ya usimamizi mzuri wa uchumi. Najua mabadiliko yanaweza kuwa ajenda ya
malengo yetu, lakini kuna sababu nzuri kwa sisi kuwa na nia.”
“China imeweza katika siku za nyuma, sisi
pia tunaweza kufanya sasa, lakini tunahitaji kuungwa mkono,” alisema Samia.
Aidha, alisema uhusiano kati ya China na
Tanzania ni wa muda mrefu na kwamba wanathamini mchango mkubwa wa China katika
maendeleo ya Tanzania.
Akizungumzia nyanja ya kisiasa, alisema
ubadilishanaji uzoefu baina ya nchi hizo mbili hasa katika masuala ya utawala,
umeongezeka na kuzaa matunda.
Alisema ziara ya hivi karibuni ya Waziri wa
Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, ilikuwa si tu kwajili ya kuboresha mahusiano ya
kidiplomasia pekee, bali pia kufanya kazi ya kuweka mazingira mazuri kwa ajili
ya utekelezaji wa miradi na mikakati ya miradi ya miundombinu, ambayo ni muhimu
katika kusaidia maendeleo ya viwanda nchini.
Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing
alisema sikukuu hiyo muhimu, wamefanya hivyo ili kuruhusu Watanzania kujua
utamaduni wa Wachina, huku akitoa shukrani kwa Serikali kwa msaada na
ushirikiano.
Alisema, mwaka uliopita ulikuwa ni muhimu
kwa ajili ya mahusiano ya China na Tanzania na pia ni mwaka wa kwanza wa
utekelezaji wa matokeo ya Mkutano wa FOCAC uliofanyika jijini Johannesburg,
Afrika Kusini.
Alisema chini ya uongozi wa Rais John
Magufuli, Serikali ya Tanzania inasisitiza mapambano dhidi ya rushwa na uvivu,
na kuhimiza uwajibikaji ili watu wote waweze kunufaika.
Alisema kwamba Rais Magufuli alianza kwa
kuchukua hatua madhubuti za mfululizo, kukomesha matatizo hayo. Balozi Youqing
alisema Rais Magufuli alimuandika barua Rais wa China, Xi Jingping na watu wa
China, kumpongeza kwa mafanikio ya Serikali ya China iliyopata katika mapambano
ya rushwa na kufanya mageuzi ya kina.
“Alisifu uhusiano wa kindugu kati ya
Tanzania na China, alisisitiza kwamba ushirikiano wa Tanzania na China, na
mpango wa “Belt and Road” utasaidia maendeleo ya viwanda nchini Tanzania na
alisema Tanzania itaendelea kuinga mkono China katika masuala mbalimbali,”
alisema Balozi Youqing.
Aliongeza kuwa China inafurahia ushirikiano
wa kina katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kimataifa. Kwamba
katika uwanja wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, China imekuwa
mkandarasi mkubwa na chanzo cha pili kwa uwekezaji. Alitaja baadhi ya miradi
mikubwa ni reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Bandari ya Bagamoyo na hifadhi
ya viwanda Buguruni; na mradi wa biashara ya muhogo pia uko kwenye ukuaji
mzuri.
Alisema Ubalozi wa china nchini utatekeleza
kikamilifu makubaliano ya mawaziri wawili ambao ni Wang Yi wa China na Dk
Augustine Mahiga wa Tanzania ili kuendeleza mahusiano kwa manufaa ya nchi hizo
mbili. Balozi huyo pia alisema ubalozi wake, umechangia Sh milioni 100 katika
Mfuko wa Maendeleo ya Serikali, ili kusaidia sekta ya elimu nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema Tanzania imepewa kipaumbele cha
kipekee katika nchi za Afrika, kwakuwa China imetoa dola za Mareakni milioni 60
kwa ajili ya kusaidia nchi za Afrika na imechagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza
kati ya nne, ambazo ni Afrika Kusini, Ethiopia na Kenya.
Alisema kama ulivyo mwaka huo wa Jogoo,
mahusiano ya China na Tanzania nayo yanazidi kuwika katika nyanja mbalimbali.
“…Katika hili la viwanda China imeahidi kama sisi tutachangamkia fursa hizo,
viwanda vingi vidogovidogo na vile ambavyo sasa hivi vinachukua ajira ya watu
wachache, kwasababu wao wanajikita katika teknolojia kubwa, viwanda hivyo
vitahamia Tanzania,” alisema Dk Mahiga.
No comments