CCM ZANZIBAR KUWATUMBUA VIONGOZI WANAOKIUKA MAADILI
Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai
akitoa mada ya Muelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa CCM mwaka 2017/2022 katika
mafunzo maalum ya siku Moja ya viongozi na watendaji wa chama hicho ngazi za
matawi, wadi na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja kichama
Washiriki
wa Mafunzo hayo ambao ni Viongozi na watendaji wa chama hicho ngazi za matawi,
wadi na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja kichama.
Na
Is-haka Omar , Zanzibar.
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewaonya baadhi ya viongozi na wanachama
wanaowashutumu na kuwadhalilisha viongozi wenzao katika vyombo vya habari na
hadharani kinyume na utaratibu wa taasisi hiyo.
Onyo
hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati
akitoa mada ya Muelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa CCM mwaka 2017/2022 katika mafunzo
maalum ya siku Moja ya viongozi na watendaji wa chama hicho ngazi za matawi,
wadi na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja kichama.
Alisema
viongozi na wanachama wenye tabia hiyo ndani ya CCM hawawezi kuvumiliwa na
watachukuliwa hatua za kinidhamu kupitia vikao vya maadili vya chama hicho
endapo watathibitika kukutwa na hatia ya kuwajibika.
Alifafanua
kwamba Chama hicho kikiwa ndio kinara wa Demokrasia katika mfumo wa vyama vingi
Tanzania, utamaduni wa kukosoana, kuelekezana , wajibishana na kufanya maamuzi
mazito kwa baadhi ya mambo yasiyokwenda sawa kimaadili na kiuongozi upo lakini
kwa kufuata utaratibu wa vikao rasmi vya kikanuni ndani ya chama na sio
hadharani.
“
Kuna tabia imezuka kwa baadhi ya viongozi na wanachama ndani ya CCM Zanzibar
wamekuwa wababe kiasi cha kuwashutumu viongozi wenzao shutuma nzito, tena
hadharani na kupitia vyombo vya Habari, wakati kuna fursa pana ya vikao vya
chama ambayo ndio sehemu pekee ya kuelekezana kwa lengo la kupata ufumbuzi wa
tatizo.
Tabia
hiyo hatuwezi kuivumilia lazima tukate mizizi mapema kabla haijakomaa na
kukiangamiza chama chetu, na wote wanaohusika na tuhuma hizo kwa sasa
tunawachunguza na kuwafuatilia kwa kina ili kujiridhisha na yeyote atakayekutwa
na hatia vikao vya Maadili vya chama vitachukua hatua stahiki bila ya kumuonea
mtu yeyote.” Alieleza Vuai huku akiwataka wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara
moja.
Vuai alisisitiza kauli yake na kuahidi
kuwa Chama hicho Zanzibar hakitomvumilia kiongozi yeyote
anayevunja maadili ya uongozi kwa makusudi badala yake kitamshughulikia bila kujali cheo na umaarufu wake kisiasa.
Aliziagiza
Kamati za Maadili kwa ngazi mbali mbali katika maeneo yaliyozuka migogoro hiyo
kuanza mara moja kutekeleza wajibu wao wa kuwaita viongozi hao katika vikao vya kikanuni ili kusuluhisha na
ikishindikana wafuate utaratibu na kuwapeleka katika ngazi zingine za maamuzi.
Alitoa
wito kwa viongozi na watendaji wa Chama na jumuiya zake pamoja na wanachama kwa
ujumla kusoma Ibara ya 18 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2012
inayoelekeza kuwa ni Mwiko kwa kiongozi
“ Kutumia madaraka aliyopewa ama kwa ajili ya manufaa yake binafsi au
kwa upendeleo , au kwa namna yoyote ambayo ni kinyume cha lengo lililokusudiwa
madaraka hayo”., alinukuu kifungu hicho Vuai.
Naibu
Katibu Mkuu huyo akizungumzia mulekeo wa CCM aliwataka viongozi, watendaji na wafuasi wa Chama hicho
kujiandaa kikamilifu kukabiliana na mabadiliko ya muundo mpya wa Chama na
Jumuiya zake.
Alisema
mabadiliko hayo yanatokana na kikao Cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichokaa
Disemba 13 mwaka 2016, kufikia maamuzi ya kupitisha mapendekezo ya Kamati Kuu
ya kufanya mabadiliko ya muundo wa Chama hicho.
Vuai
alieleza kuwa lengo la kufanyika kwa
mabadiliko ya muundo wa chama ni kuimarisha uhai wa taasisi hiyo kiutendaji na
kiuongozi ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kulingana na wakati uliopo sasa katika
ushindani wa kisiasa.
Hata
hivyo aliyataja baadhi ya mapendekezo yaliyofikiwa katika Kikao hicho kuwa ni
pamoja na kupunguza idadi ya wajumbe na vikao ambayo kwa sasa ni kubwa na
inafanya chama hicho kishindwe
kutekeleza vizuri baadhi ya majukumu yake.
“
Wajumbe tulitafakari kwa kina muelekezo wa CCM, mienendo ya kiutendaji ya
watumishi na viongozi pamoja na mahitaji
halisi ya wanachama wetu tukaona kuna haja ya kufanyika mabadiliko ili tutabane matumizi kwa kupunguza baadhi ya gharama
zisizokuwa za msingi ndani ya chama.
Ili
chama chetu kiendelee kuwa mwalimu wa Demokrasia ndani na nje ya Tanzania
lazima wanachama wote tuwe wamoja na wenye mshikamano katika kuunga mkono
juhudi za kuleta mabadiliko yenye ufanisi
kiutendaji ndani ya chama hicho.”, alielza Vuai.
Naibu
Katibu Mkuu huyo alifafanua baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na kikao hicho
kuwa yaliamua kupunguza Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka 388 na
kupendekezwa wawe 158 kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Kwa
upande wa ngazi ya Kamati Kuu walipendekezwa wawe wajumbe 24 badala 34 ambapo
kati ya hao wajumbe watatu watachaguliwa na Halmashauri Kuu kutoka Tanzania
bara na watatu wengine watachaguliwa na Halmashauri kuu ya Zanzibar.
Alisema maandalizi ya kufanyika kwa muundo
huo ndani ya Chama yalianza zamani kwani yalikuwa yafanyike mwaka 2012,
na kuhairishwa kutokana na sababu zisizoweza kuepukika.
Alisema
baada ya kuhairishwa kufanyika kwa muundo
huo chama kiliendelea
kujipanga kwa kuwashirikisha wataalamu
wa masuala ya kisiasa, kutoka Vyuo ili
watathimini na kutoa ushauri wa
kitaalamu utakaozaa muundo unaokidhi mahitaji ya wanachama.
Alibainisha
kuwa Mapendekezo hayo yatapelekea kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ya Chama
na kanuzi za jumuiya na chama, na kuongeza kuwa vyeo ambavyo havitokuwemo katika
Katiba hiyo havitoruhusiwa ndani ya Chama jumuiya.
Vuai
aliwataka viongozi wanaohusika na vikao
vya kuchuja waombaji wa nafasi za uongozi kufuata maadili ya kikanuni kwa
kuhakikisha, muombaji ametimiza masharti ya uanachama kwa mujibu wa ibara ya 8 ya
Katiba ya CCM.
Alitoa
angalizo kwa wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanachagua viongozi wenye
uwezo, waadilifu na waumini wa kweli wa
CCM watakaoweza kusimamia maslahi ya Chama kwa vitendo.
“
Tutumie vizuri fursa hii ya uchaguzi kwani ndio sehemu pekee ya kupata timu
imara ya kuongoza jahazi la CCM kwa ufanisi na mafanikio makubwa kwa miaka
mitano ijayo.
Pia
ngazi husika hasa Kamati za siasa kwa ngazi mbali mbali lazima mtoe taarifa na
matangazo mapema kwa wanachama ili
waweze kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi kwani ni haki ya kikatiba
kwa kila mwanachama kuchagua na kuchaguliwa
’’ Alisisitiza kiongozi huyo.
Aidha
aliwataka wabunge, wawakilishi na madiwani kutengeneza mazingira rafiki ya
upatikanaji kwa urahisi fursa za Mikopo na mafunzo ya Ujasiriamali kutoka
katika taasisi zinazozihusika na masuala ili ziweze kuwasaidia vijana ambao
hawapo katika mfumo rasmi wa ajira na waweze kujiajiri wenyewe.
Nao
Washiriki wa Mafunzo hayo waliwashauri viongozi na Watumishi wa CCM na Jumuiya
zake wa ngazi za Juu kuonyesha mfano wa kiutendaji ili viongozi na wanachama wa
ngazi za chini waweze kufuata nyayo hizo kwa vitendo.
Walisema
licha ya Mkoa huo kuwa na fursa ya Hoteli nyingi za Kitalii na rasilimali ya
bahari bado kundi la vijana wanakabiliwa
na tatizo la upungufu wa ajira, jambo linalotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa
kudumu na serikali kwa kushirikiana na Chama.
Mafunzo
hayo ya siku moja yamewashirikisha jumla ya
viongozi na watendaji 487 wa chama na jumuiya wa ngazi za matawi, wadi
na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini “B” kichama.
No comments