TAARIFA KWA UMMA: SERIKALI YATOA TAHADHARI KUHUSU MAFUA YA NDEGE
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto imewatahadharisha Watanzania juu ya kuwapo kwa virusi vya ugonjwa wa
mafua ya ndege.
Ugonjwa
huo umegundulika kuwapo katika nchi jirani ya Uganda ambako taarifa zinaeleza
kuwa maeneo yaliyoathirika ni yale yanayozunguka Ziwa Victoria.
Tahadhari
hiyo imetolewa jana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kupitia taarifa yake
iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Serikalini- Afya.
“Ugonjwa
huu umegundulika baada ya kuwapo kwa vifo vingi vya ndege pori katika maeneo ya
Lutembe Beach, Masaka, Kachanga, Bukibanga na Bukakata nchini Uganda.
“Vilevile,
vifo hivi vimetokea kwa baadhi ya ndege wafugwao (kuku na bata) na inahisiwa
kuwa ndege hao wamepata virusi vya ugonjwa huo kutoka kwa ndege pori wanaohama
kutoka nchi za Ulaya,” alisema.
Waziri
Ummy alisema vifo hivyo vya ndege pori vilianza kuonekana tangu Januari 2,
mwaka huu na vimeonekana kuendelea hadi sasa.
“Kwa
hapa nchini hakuna vifo vya ndege vilivyoripotiwa hadi sasa,” alisisitiza.
Alisema
ingawa hadi sasa hakuna binadamu aliyeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo
nchini Uganda, tahadhari inatolewa kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kusambaa
kwa binadamu ikiwa hatua madhubuti za kujikinga hazitazingatiwa.
Waziri
Ummy alisema ugonjwa huo unasababishwa na virusi aina ya Influenza na huenezwa
na ndege pori wanaohama hama.
Alisema
ndege hao hubeba virusi vya ugonjwa huu bila ya kuonesha dalili za ugonjwa.
“Hivyo
huweza kuambukiza ndege wanaofugwa majumbani mfano kuku na bata wakati
wanapokutana nao. Aidha ndege hao huweza kuambukiza ugonjwa kupitia njia ya
kinyesi ambacho hudondoshwa ardhini au kwenye mabwawa na madimbwi ya maji,”
alisema.
Aliongeza:
“Kwa kuwa binadamu huwezaa kuambukizwa ugonjwa huu kwa kugusana na ndege au
kinyesi cha ndege aliyeathirika na ugonjwa huu. Ni muhimu kutokugusa mizoga ya
ndege pori au kinyesi chake.”
Alisema
kuwa binadamu anaweza pia kupata maambukizi wakati wa kuchinja kuku, kunyonyoa
manyoya, na wakati wa kutayarisha kabla ya kumpika.
Waziri
Ummy aliwataka wananchi watoe taarifa iwapo wataona dalili zozote za ugonjwa na
vifo katika jamii ya ndege wa kufugwa na ndege pori.
“Kuna
uwezekano wa virusi hivi kuambukizwa kutoka kwa binadamu mwenye uambukizo
kwenda kwa binadamu mwingine, na hii ikitokea inaweza kusababisha mlipuko
mkubwa unaoweza kusambaa pande zote za dunia,” alisema.
No comments