MSAJILI WA VYAMA AIBUKA , ASHIKILIA MSIMAMO WAKE WA KUMTAMBUA PROF LIPUMBA KAMA MWENYEKITI WA CUF
Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema hana hofu ya
kuchafuliwa kutokana na tuhuma zinazotolewa dhidi yake, huku akisema msimamo
wake uko palepale na kwamba anamtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti
wa CUF na Maalim Seif ni Katibu Mkuu.
Kauli
ya Jaji Mutungi imekuja baada ya taarifa na kauli za matusi na kejeli
zilizomuhusisha yeye na ofisi yake kusambaa kwenye mitandao mbalimbali ya
kijamii baada ya kuidhinisha zaidi ya Sh300 milioni za ruzuku kwenda kwenye
akaunti ambayo kamati ya uongozi ya CUF ilidai siyo ya chama hicho.
Taarifa
za msajili kuingiza fedha hizo kwenye akaunti hiyo na baadaye kutolewa kwa njia
ambayo inaonekana kutia shaka zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya
CUF, Julius Mtatiro ambaye alilinganisha suala hilo na uchotwaji wa zaidi ya
Sh300 bilioni zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Kupitia
taarifa yake jana, Jaji Mutungi alisema kuna mbinu zinazopangwa na wanaojiita
Kamati ya Uongozi ya CUF ambayo ofisi yake haiitambui, huku akisisitiza
kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa CUF na Maalim Seif kuwa Katibu
Mkuu.
Jaji
Mutungi ambaye mwishoni mwa mwaka jana alifunguliwa kesi Mahakama Kuu na bodi
ya wadhamini wa CUF ikiiomba itoe amri ya kubatilisha barua ya mlezi huyo wa
vyama vya siasa inayomtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF, alisema
kauli zinazotolewa mitandaoni zina lengo la kuchafua ofisi yake.
Msajili
huyo alisema moja ya mkakati huo ni taarifa iliyosambazwa juzi na Kaimu Naibu
Mkurugenzi wa Habari wa CUF,, Mbarala Maharagande ya kejeli, matusi, tuhuma na
dhihaka kwake.
Jaji
Mutungi alisema hivi karibuni, Maharagande alizungumza na waandishi wa habari
huku akidai kuwa ofisi ya msajili inasababisha mpasuko ndani ya chama hicho na
ndiyo maana imetoa ruzuku kwa Profesa Lipumba.
Licha
ya tuhuma hizo, Jaji Mutungi alisema kwamba haogopi kuchafuliwa akizingatia
ukweli kwamba yeye ni mtumishi wa umma na anafanya kazi zake akiwatumia
wananchi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alisema
kamwe hawezi kuyumbishwa na matusi wala kejeli zinazotolewa dhidi yake pamoja
ofisi anayoiongoza.
“Nimezipata
hizo taarifa kwamba kuna baadhi ya watu wamepanga kupambana nami kwa
kunichafua, japo naendelea kuzifanyia kazi lakini waache wanichafue, wala
siogopi lolote,” alisema.
Alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo, Maharagande
aliendelea kusisitiza kuwa kauli iliyotolewa wakati alipofanya mkutano na
vyombo vya habari ipo hivyo na kwamba waliitisha mkutano kumjibu msajili ambaye
alifanya mkutano na waandishi wa habari siku moja kabla kuhusu masuala ya CUF.
No comments