Breaking News

DK. MPANGO: AWATAKA WATANZANIA KUNUNUA HISA ILI KUPANUA WIGO WA KUMILIKI MAKAMPUNI ZA NDANI BADALA YA KUWAACHIA WAGENI

1  Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akitoa hotuba kabla ya kuzindua rasmi Jina Jipya na Nembo ya kibiashara na Benki ya Posta Tanzania (Tpb Bank Plc), Tukio lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam.
1    Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania (Tpb Bank Plc), Bw. Sabasaba Moshingi, akielezea mafanikio ya Benki hiyo katika Sekta ya Fedha ambayo ni kukuza mtaji, kupata faida na kufanikiwa kubuni Jina Jipya na Nembo Mpya ya Kipepeo, baada ya kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam.
1    Dkt. Philip Mpango, (wa pili kulia), akimpongeza Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania (Tpb Bank Plc), Bw. Sabasaba Moshingi, mara baada ya kuzindua nembo mpya ,tukio lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam.
     
     Dar es salaam

Watanzania wametakiwa kununua hisa kwa wingi ili kupanua wigo wa kumiliki makampuni ya hapa nchini badala ya kuwaachia wageni.

Akizungumza katika uzinduzi wa jina jipya na nembo ya Benki ya Posta (TPB Bank PLC) uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Uchumi Dk. Philip Mpango alisema watanzania wamekuwa wakilalamika kuhusu umiliki wa makampuni ya ndani huku wakishinda kununua hisa na kuwaachia wageni  wakimiminika kwa wingi.

“Naomba watanzania wanunue hisa za TPB Bank, tujifunze na sisi sasa kushiriki kikamilifu katika soko la hisa na ndio umiliki wenyewe, tusingoje kuita watu wengine waje kuona umuhimu wa hisa,” alisema Dk. Mpango.

Aidha Dk. Mpango alisema watanzania wamekuwa wabunifu hususani wanawake lakini changamoto kubwa imekuwa mtaji lakini kwa ujio mpya wa TPB Bank changamoto hiyo itaweza kutatuliwa kwa pamoja na serikali.

Hata hivyo alisisitiza kuwa watanzania wanapaswa kujengwa utamaduni wa kujiwekea fedha za akiba katika mabenki kutokana na maendeleo makubwa ya sekta ya kibenki nchini ambao utawasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kimaisha.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa TPB Bank Sabasaba Moshingi alisema hadi mwaka 2011 kulikuwa na idadi ndogo ya watanzania wanaotumia huduma za kibenki lakini ubunifu ambao umefanyika hadi hivi sasa umeongeza matawi ya benki hiyo kutoka 28 hadi kufikia 60.

Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Profesa Lettice Rutashobya alimhakikishia Waziri wa fedha kuwa benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake hususani kwa watanzania walioko pembezoni ili nao waweze kufaidika na huduma zake.

TPB Bank ilianzishwa mwaka 1925 ambapo mwaka 1991 iliingia katika mfumo wa kujitegemea ambapo Machi 23 mwaka jana ilisajiliwa na kuruhusiwa kutumika kwa jina la TPB Bank PLC.


No comments