KATIBU WA CHADEMA APOTEZA FAHAMU BAADA YA KUSHUSHIWA KICHAPO NA VIJANA WA CCM
Katibu
wa Chadema Jimbo la Sengerema, Deusdeth Mwigala juzi, alipata kipigo kutoka kwa
vijana wa CCM kilichosababisha apoteze fahamu baada ya kutuhumiwa kutaka
kuvuruga mkutano wa hadhara.
Kiongozi
huyo wa Chadema alikuwa akipita karibu na eneo ambalo CCM walikuwa wakiendelea
na mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Kahumulo, akiwa
na vipaza sauti alivyotumia kutangaza mkutano wa chama chake, kitendo
kilichotafsiriwa kuwa ni kuvuruga usikivu.
Hata
hivyo, katibu huyo alikana kuvuruga mkutano wa chama hicho akidai alikuwa
umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka eneo ambalo CCM ilikuwa ikiendesha mkutano.
“Wakati
naendelea na kazi ya kutangaza mkutano wa Chadema nikiwa nimeongozana na makada
wengine wanne na dereva, ghafla tulivamiwa na watu wa CCM na wakaanza
kutushambulia,” alisema Mwigala akizungumzia tukio hilo lililotokea Kijiji cha
Lubanda.
Alisema
wenzake pamoja na dereva walifanikiwa kukimbia, lakini yeye alinaswa na wafuasi
hao walioendelea kumshambulia kwa kipigo.
Hata
hivyo, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, James Kisinza alimtupia lawama katibu
huyo wa Chadema kwa kitendo cha kupita karibu na eneo la mkutano wa CCM
akitangaza mkutano wa chama chake kwa kutumia vipaza sauti na hivyo kuvuruga
usikivu.
Katibu
wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani Sengerema, Hassan Moshi alisema
wafuasi wao walichukizwa na kitendo hicho na kuamua kumuadhibu kiongozi huyo
kwa madai kuwa alikuwa anavuruga mkutano wao kwa makusudi.
“Viongozi
tulilazimika kuingilia kati kumwokoa asiendelee kuadhibiwa na vijana wenye
hasira, lakini ukweli ni kwamba mwenzetu alifanya kosa kwa kuingilia mkutano wa
chama kingine kinyume cha sheria,” alisema Moshi.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema ofisi yake haijapokea taarifa
hizo na kuahidi kuzitolea ufafanuzi baada ya kuzipokea kutoka Sengerema.
credit Malunde
No comments