HOSPITALI YA MUHAS MLOGANZILA, KUPUNGUZA FOLENI YA WAGONJWA MUHIMBILI.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Sekta
ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni sekta muhimu sana
katika kujenga uchumi wa nchi kwani bila rasilimali watu wenye afya njema, nchi
haiwezi kuwa na uchumi ulio imara.
Katika
kuimarisha rasilimali watu itakayochochea maendeleo ya nchi, Serikali ya awamu
ya tano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inajitahidi kuhakikisha huduma za
afya za uhakika zinatolewa kwa wingi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa
kutambua umuhimu wa suala hilo, Serikali ilianzisha ujenzi wa Hospitali ya
kisasa katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) kilichopo eneo
la Mloganzila nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ambayo tayari imekamilika na
inatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2017.
Ujenzi
wa Hospitali hiyo ya kipekee na ya aina yake katika eneo la Afrika Mashariki na
kati ulianza mnamo Aprili 24 mwaka 2104 na kukamilika Agosti 31 mwaka 2016
ambapo kwa sasa wataalamu wanaendelea kuweka vifaa tiba na kufunga mifumo ya
vifaa vya tehama ili kurahisisha kazi hospitalini humo.
Hospitali
hiyo ya kisasa ilijengwa kwa mkopo wa riba nafuu kutoka Serikali ya Korea
Kusini pamoja na fedha ya Serikali ya Tanzania hivyo hadi kukamilika kwake
imegharimu jumla ya dola za kimarekani milioni 94.5 ambazo ni sawa na Tsh.206.7
bilioni.
Kaimu
Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Muhimbili), Eligius Lyamula amesema kuwa Serikali
iliamua kutoa kiwanja chenye ukubwa wa hekari 3800 kwa ajili ya kupanua
shughuli za Chuo na kuweza kuzalisha wataalam wa kada mbalimbali za afya ili
kuweza kutatua changamoto za afya zinazowakabili wananchi.
“Hospitali
hii ina uwezo wa kuweka vitanda 571 na inategemewa kutibu magonjwa makubwa
hivyo tunategemea kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali
yetu ya Taifa ya Muhimbili pamoja na kupunguza gharama kwa wanaoenda kutibiwa
nje ya nchi,” alisema Lyamula.
Aliongeza
kuwa Hospitali hiyo inategemea kutoa huduma za kisasa pamoja na kutoa mafunzo
kwa wanafunzi wanaosomea sekta ya afya ili kuondokana na tatizo la upungufu wa
watumishi wa kutosha katika sekta ya afya na wasio na ujuzi katika taaluma
hiyo.
Lyamula
alifafanua kuwa Serikali iliona tatizo la upungufu wa watumishi wa afya hivyo
ikaamua kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga chuo hicho ambacho kitakuwa na
uwezo wa kudahili wanafunzi 15,000 kutoka wanafunzi 4000 wanaodahiliwa kwa sasa
hivyo ni dhahiri kabisa kuwa wagonjwa watapata huduma za uhakika.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh.Paul Makonda alipotembelea Chuo
hicho mnamo Novemba 26 mwaka 2016 kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa
chuo hicho alitoa ushauri kwa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto kuweka sheria kwa wanafunzi wanaosomea masomo hayo kwa mkopo kupewa
sharti la msingi la kufanya kazi katika hospitali za umma kwa miaka isiyopungua
mitatu.
Hiyo
yote ikiwa ni njia ya kutatua changamoto ya watumishi wa afya katika hospitali
za Umma kwani imeonekana kuwa wanafunzi wengi wa kada hiyo humaliza vyuo na
kukimbilia kufanya kazi katika hospitali za binafsi au nje ya nchi na kuacha
hoapitali hizo zikielemewa na idadi kubwa ya wagonjwa.
Mhe.
Makonda alikaririwa akisema kuwa,” wanafunzi wanaosoma sekta ya afya kwa mikopo
wanatumia bajeti kubwa ya Serikali na hizo zote zikiwa ni fedha za kodi za
wananchi lakini mwisho wa siku wanaondoka bila kuwatumikia wananchi hao
waliojitolea fedha zao kuhakikisha wanapata elimu”.
Aidha,
Mhe Makonda aliupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kutenga eneo kwa ajili ya
viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na eneo litakalotumika kujenga kituo
kikubwa cha utafiti wa masuala ya sayansi na liahidahidi kusaidiana nao kwa
hali na mali katika kuhakikisha ujenzi wa chuo hicho unakamilika.
Njia
nyingine ya kuhakikisha kuna kuwa na watumishi wa kutosha katika hospitali hiyo
inayotarajiwa kuwa na watumishi 1300 ni kuhamisha watumishi kutoka katika
hospitali mbalimbali nchini ambapo kwa kuanzia watumishi 928 wa awali
wameshahamishiwa Hospitalini hapo.
Katika
mkakati wa kuhakikisha wanaongeza idadi ya watumishi ili kuijengea uwezo na
ufanisi hospitali hiyo serikali imetoa kibali cha kuajiri watumishi 50 katika
mwaka wa fedha wa 2016-17 na wataendelea
kuajiri kadiri bajeti itakavyoruhusu.
Kwa
upande mwingine, Serikali imeamua kuweka historia nyingine ya kujenga kituo cha
utafiti, mafunzo na tiba za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kitakachojengwa
ndani ya eneo hilo la Mloganzila ambapo ujenzi huo unategemewa kuanza mnamo
mwezi Mei mwaka 2017.
Mbali
na kuongeza watumishi wa afya wenye weledi na kupunguza adha ya foleni katika
hospitali zingine, nchi yetu pia itanufaika kwa kuwa na kituo hicho cha utafiti
ambacho kitakuwa kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ujenzi
huo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika
(ADB) ambapo kwa awamu ya kwanza ya mradi Serikali imetoa jumla ya shilingi
7,055,000 na ADB imetoa mkopo wa jumla ya shilingi 9,500,000.
Pia,
ili kuhakikisha nchi yetu inapunguza gharama za wananchi kwenda kutibiwa nchi
za nje, Serikali itachagua jumla ya wataalam 24 kutoka kada mbalimbali za
magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa ajili ya kupewa mafunzo ya kina kuhusu
magonjwa hayo katika hospitali za nje na ndani ya nchi ili waweze kubobea
katika kutibu magonjwa hayo hivyo kupelekea wagonjwa kutibiwa hapa hapa nchini.
Kaimu
Makamo Mkuu wa chuo hicho, Lyamula anaendelea kusema kuwa baada ya ujenzi huo
kukamilika, uongozi wa chuo unajitahidi kwa hali na mali kutafuta mikopo na
misaada mbalimbali nje na ndani ya nchi ili kuweza kuendeleza eneo lililobakia
kwa ajili ya ujenzi wa chuo ambao ndio litakua chimbuko la wataalamu wa afya
wenye utaalamu wa kutosha.
Aidha,
alifafanua kuwa jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 510,696,243 zinaendelea
kutafutwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za waalimu, madarasa, maktaba, majengo
ya utawala, mabweni ya wanafunzi, kumbi za mikutano pamoja na maabara.
Mkatati
wa uboreshaji wa huduma za afya nchini hauishii tu kwenye kujenga hospitali
mpya na za kisasa bali pia kuboresha maslahi ya wafanyakazi ili waendane na
umuhimu wa kazi wanayoifanya kwaajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Kwakuwa
suala la afya ni suala mtambuka ambalo wadau wengi wa maendeleo wanatakiwa
kushiriki ni vyema hata sekta binafsi ikaiunga mkono serikali kwa kupeleka
huduma za afya kwenye maeneo ambayo hazipatikani ili kuweza kusaidiana na
Serikali katika kufanikisha adhma ya kuwa na huduma bora za afya kwa wananchi
hasa katika maeneo ya vijijini.
No comments