Breaking News

SHEREHA ZA MIAKA 55 YA UHURU WA TANZANIA BARA


Wakati Tanzania Bara ikielekea kuadhimisha miaka 55 ya uhuru wake hapo kesho, jamii ya Watanzania imetakiwa kujitathmini na kubadilika hasa katika kutunza mali za serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na EATV pamoja na East Africa Radio kuhusu maandalizi ya sherehe hizo.

Mhe. Jenista amesema vitendea kazi na miundombinu iliyojengwa kwa kodi za wananchi ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda na kuvithamini ili vilete mabadiliko katika kufikia malengo ya nchi.
Akizungumzia maandalizi ya sherehe za kutimiza miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania amesema tayari kila kitu kimekamilika sambamba na mialiko kwa viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa imeshawasilishwa kwa viongozi hao.

Mgeni rasmi katika sherehe hizo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 9 katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Nao baadhi ya wananchi wamesema ni wajibu wa kila Mtanzania kuungana kwa pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa pamoja na kupongeza juhudi za Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anazozifanya katika kupambana na rushwa na kusimamia maadili ya viongozi wa umma.

No comments