POLISI KANDA MAALUM DAR: YAWATIA MBARONI WATU 22 KWA KOSA LA UPORAJI KATIKA MAGARI
Kikosi maalumu cha kupambana na wizi wa kutumia
silaha na wizi wa kutumia nguvu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
kimewakamata watuhumiwa 22 kwa makosa ya kuwapora wenye magari na wapitanjia
kwenye mataa ya kuongozea magari.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo,
Simon Sirro alisema watuhumiwa hao, wamekuwa wakijiunda kwenye vikundi na
kuwanyang’anya watu wenye magari na watembea kwa miguu mali zao kama simu za
mikononi, kompyuta, saa na fedha.
Alisema
ufuatiliaji ulifanyika na kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti, ambapo
Desemba 11 mwaka huu huko Temeke maeneo ya Keko Magurumbasi na mataa ya Veta na
Chang’ombe walikamatwa watuhumiwa 10 kwa makosa ya wizi kutoka maungoni na wizi
kutoka kwenye magari.
Aliwataja
baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Ayubu Amiri (19), mkazi wa Mtoni Mtongani,
Shabani Fadhili(18) mkazi wa Keko, Herman Francis (26), mkazi wa Keko
Magurumbasi na wenzao saba.
“Katika
mahojiano watuhumiwa wamekiri kujihusisha na makosa mbalimbali yakiwemo
unyang’anyi wa kutumia silaha na kutumia nguvu,” alisema.
Aidha
alisema uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa Herman Francis anakabiliwa na
tuhuma za mauaji, ambapo Machi 20 mwaka huu alimchoma mtu kisu na kutoroka
kusikojulikana.
Wakati
huo huo, Desemba 12 mwaka huu askari waliwakamata watuhumiwa wengine 12 kwa
makosa ya wizi kutoka kwenye magari.
Watuhumiwa
hao wametajwa kuwa ni Sande Kassim (18), mkazi wa Keko, Emmanuel Abeli (21),
Paulo Abeli(18), Jafari Nyerere (22), Hamis Salum (22), Hemed Idrisa(22) wote
wakazi wa Keko na wenzao sita.
Katika
tukio lingine, polisi wamewakamata watuhumiwa wanne wanaojihusisha na wizi kwa
kuwarubuni watu kwa kukodi magari yao na baadaye hutumia nguvu kuwapora.
Watuhumiwa
hao wametajwa kuwa ni Juma Kajeni (35), mkazi wa Tabata, Hamadi Kaganda (38),
mkazi wa Mbagala, Mashaka Ally(62), mkazi wa Yombo na Mshamu Ally (32), mkazi
wa Mtongani.
Alisema
watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watapelekwa
mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.
Pia
aliwatahadharisha wananchi na wamiliki wa magari kuwa makini kwa watu hao ambao
huja kwa nia ya kuwalipa fedha nyingi au kukodi gari kwa kiwango kikubwa na
kisha wanatokomea na gari.
Wakati
huo huo, polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kupitia kikosi kazi chake cha
kupambana na wizi wa magari kimekamata magari matatu ya wizi katika mikoa
mbalimbali.
Sirro
alilitaja gari lenye namba T 386 CGY aina ya Verosa rangi nyeusi, mali ya
Abraham Robert wa jijini Dar es Salaam na gari hilo lilikamatwa mkoani Mbeya
likiwa limetelekezwa.
Gari
jingine ni lenye namba T 946 DGH aina ya IST rangi ya fedha ikiwa inaendeshwa
na mtuhumiwa aitwaye Hamadi Saidi (27) mkazi wa Kimara Dar es Salaam ambalo
lilikamatwa huko mkoani Morogoro, gari hilo liliibiwa maeneo ya Kawe Beach
jijini Dar es Salaam.
Alilitaja
gari lingine kuwa ni Mitsubishi Canter lenye namba T 753 CVZ ambazo ni namba
bandia huku namba zake halisi zikiwa ni T.815 DJF mali ya Magreth iliibiwa
maeneo ya Kimara Suka jijini Dar es Salaam.
Alisema
mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa anaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika
atapelekwa mahakamani.
Pia
alisema watuhumiwa wengine waliohusika
na wizi wa magari hayo wanaendelea kutafutwa ili kubaini mtandao mzima wa wizi
wa magari na watuhumiwa wengine wanaotafutwa kwa wizi wa magari hapo nyuma
ambao walikimbia.
|
No comments