KUFATIA UBADHILIFU WA 642 MIL, WAZIRI MKUU MAJALIWA AMTUMBUA MWEKAHAZINA WA WILAYA YA BAHI, AAGIZA ARUDISHWE LONGIDO KUJIBU TUHUMA
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amemsimamisha kazi aliyekuwa Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya
Longido, Bw. Issai Mbilu ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bahi mkoani
Dodoma na kuagiza arudishwe haraka na kuja kujibu tuhuma za ubadhilifu sh.
milioni 642.4 za miradi zinazomkabili.
“Tunaendelea kudhibiti
na kuweka nidhamu ndani ya Serikali. Ukiharibu Longido usitegemee kuhamishiwa
wilaya nyingine tunamalizana hapa hapa. Hatuwezi kuhamisha ugonjwa hapa na
kuupeleka wilaya nyingine hivyo Mwekahazina huyu arudishwe haraka Longido,” amesisitiza.
Waziri Mkuu ametoa agizo
hilo jana Ijumaa, Desemba 16, 2016 wakati akizungumza na watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa katika
ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Pia amemuagiza Katibu
Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Richard Kwitega kumuandikia barua Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akimuomba
amrudishe Mwekahazina huyo katika kituo chake cha kazi cha zamani ili aweze
kujibu tuhuma zinazomkabili.
Amesema Serikali haitamvumilia
mtumishi wa idara yoyote atakayeharibu jambo halafu kuhamishwa sehemu nyingine,
“hivyo naagiza kuanzia sasa nimemsimamisha kazi Mwekahazina huyu na arudi hapa
kujibu kwanini ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie watumishi wengine hili
liwe funzo kwenu,” amesema.
Amesema miradi mingi ya
maendeleo inakwama kwa sababu ya baadhi ya watumishi kuweka mbele maslahi
binafsi badala ya kuzingatia maadili ya utumishi, hivyo amewaagiza Wakuu wa
Idara wafuatilie kwa makini miradi inayotekelezwa katika maeneo yao kama
inalingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.
Akizungumzia kuhusu
kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya wilayani Longido, Waziri Mkuu
amewaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kufanya kufanya
msako wa nyumba hadi nyumba na kuwakamata wote watakaokutwa wanafanya biashara
hiyo.
“Wilaya hii ina sifa
mbaya ya kuwa kitovu cha kusafirisha dawa ya kulevya zikiwemo bangi na mirungi.
Hivyo nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama waendeshe msako kwa kila
nyumba na atakayekamatwa achukuliwe hatua. Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu
kazi ya Taifa,”.
“Ukivuta bangi
unapishana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu kwani unakwenda kulala jambo ambalo
hatuwezi kulikubali. Watakaokutwa wanauza au kununua mirungi na bangi wakamatwe
na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kutaifisha magari yanayotumika
kubeba bidhaa hiyo haramu,” amesema.
Awali, Mkuu wa Wilaya
hiyo Bw. Daniel Chongolo akisoma Taarifa ya Wilaya amesema Longido inakabiliwa
na changamoto mbalimbali ikiwemo kutumika kama njia kuu ya kusafirisha dawa za
kulevya aina ya bangi na mirungi kwenda nchi jirani ya Kenya ambako biashara
hiyo imehalalishwa.
Changamoto nyingine ni
ukosefu wa hospitali ya wilaya hali inayofanya wananchi kwenda kutibiwa Kenya,
ambapo Waziri Mkuu alisema haiwezekani wakakosa hospitali ya wilaya hivyo
amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikiusha anatenga fedha za ujenzi
huo.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema Serikali ipo mbioni kujenga kiwanda cha kuchakata madini ya
magadi soda ili yawe na ubora na thamani kubwa. Ametoa kauli hiyo
aliposimamishwa na wananchi katika kijiji cha Loonolwo kilichopo Kata ya Gelai
Merugoi Wilayani Longido akitokea wilayani Ngorongoro.
Amesema lengo la kujenga
kiwanda hicho ni kuwawezesha wananchi wa wilaya hiyo hasa akinamama wanaoishi
karibu na Ziwa Natron linalotoa magadi hayo waweze kunufaika na uwepo wa ziwa
hilo.
Waziri Mkuu amesema
ujenzi wa kiwanda hicho utawezesha vijana na akinamama hao wanaouza magadi
maeneo ya pembezoni mwa barabara katika ziwa Natron kupata ajira kwa kuwa
kitazalisha ajira zaidi ya 500 katika wilaya hizo mbili za Longido na
Ngorongoro.
Pia amemuagiza Mkuu wa
Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo kushirikiana na wataalam wake kufanya
tathimini ya uhaba wa chakula katika wilaya za Longido na Ngorongoro ili
Serikali ijue Mkoa wa Arusha una ukosefu wa chakula kwa kiasi gani.
"Gambo fanya
tathimini ya hali ya njaa katika wilaya hizi mbili ili tuweze kuwasaidia
wananchi hawa. Hata hivyo nawaomba wananchi mtunze kiasi cha chakula
mlichonacho na marufuku tumia nafaka kwa ajili ya kupika pombe,” amesema.
Awali, wananchi hao
waliokuwa na mabango mbalimbali walilalamikia kero ya mipaka ya ardhi kati ya
vijiji vya wilaya za Longido na Ngorongoro, ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Afisa
Ardhi Mkoa wa Arusha, Bw. Hamdoun Mansour kwenda katika vijiji hivyo vya
mpakani na kukutana na viongozi wa kimila ili kumaliza mgogoro huo.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
No comments