Breaking News

KIWANGO CHA UKOSEFU AJIRA NCHINI CHAFIKIA ASILIMIA 11.7

KIWANGO cha ukosefu wa ajira kwa vijana nchini ni asilimia 11.7 huku Kenya ni asilimia 17.3, Bunge limeelezwa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde amesema, kiwango cha ukosefu wa ajira nchini imetokana na utafiti wa nguvu kazi uliofanywa mwaka 2014.

Mavunde alieleza mkakati wa kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ni kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kukuza ujuzi nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo yatakayofanyika maeneo ya kazi.

Pia serikali imeanzisha programu maalumu ya kutambua ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi na kuurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale watakaobainika kuhitaji na kuwapa vyeti.

“Ili kuthibitisha hilo kwa sasa serikali inaendelea kufundisha vijana 400 katika kiwanda cha Took Garment ikiwa lengo ni vijana 1,000, za mafunzo mengine yataanza Novemba mwaka huu katika kiwanda cha Mazava Fabrics Morogoro, DIT Mwanza kutengeneza viatu na bidhaa za ngozi, VETA nchi nzima watafundishwa vijana elfu nne,” alisema.

Mavunde alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Neema Mgaya (CCM) aliyetaka kufahamu serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la vijana wengi kukosa ajira.

Naibu Waziri huyo alitaja mikakati mingine ya kupunguza tatizo hilo kuwa ni kuwezesha vijana kuwa wajasiriamali kwa kuwatambua vijana na mahitaji yao katika ngazi mbalimballi na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi ya vijana.

Vilevile kuwahamasisha vijana wenye utaalamu kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususan kilimo biashara.

Alisema serikali itajikita zaidi kuhamaisha vijana na kuwawezesha kuwekeza kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikia lengo la asilimia 40 ya nguvu kazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020 kupitia Mpango wa pili wa Maendeleo wa miaka mitano.

“Kuendelea kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao kupitia Mfuko huo vikundi vya vijana 6,076 vyenye wanachama 30,380 vimepata mikopo yenye masharti nafuu ya Sh bilioni 1.6 kupitia kwenye Saccos zao za halmashauri za wilaya kuwawezesha vijana kupata mikopo ya masharti nafuu na kujiajiri,” alisema.

No comments