SERIKALI YAFUTA USAJILI WA MAGAZETI 473
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akizungumza na vyombo kuhusu kufutwa kwa
usajili wa magazeti 473 ambayo hayajachapishwa kwa muda wa miaka mitatu
mfululizo leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni kaimu Mkurugenzi Idara ya Habari
Bibi. Zamaradi Kawawa na Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria Bi. Flora
Mwenyembegu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akionesha kwa waandishi wa habari tangazo la serikali Na. 65 linaloonesha kusudio la kufuta viapo vya usajili wa magazeti ambayo hayajachapishwa kwa muda wa miaka mitatu kwa mujibu wa sheria ya magazeti. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria Bi. Flora Mwenyembegu
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Waziri waHabari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye (hayupo pichani), kuhusu kufutwa kwa usajili wa magazeti 473 ambayo hayajachapishwa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo jijini Dar es Salaam
Na: Frank Mvungi –
Maelezo
Serikali
imefuta usajili wa magazeti 473 kupitia tangazo lake lililochapishwa katika
Gazeti la Serikali lenye namba 195, (Supplement No. 23) la tarehe 10/06/2016
kutokana na Magazeti hayo kutochapishwa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape
Nnauye wakati akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam.
Mhe.
Nnauye alifafanua kuwa kutokana na kufutwa kwa viapo vya usajili wa magazeti
hayo, mtu yeyote atakayechapisha au kusambaza magazeti yaliyotajwa katika
tangazo hilo kwa njia ya nakala ngumu au kieletroniki atakuwa anakiuka sheria
ya magazeti sura ya 229 kifungu cha 6 na hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa
sheria.
“Iwapo
kuna mmiliki wa gazeti ambaye angependa kuendelea na biashara hii baada ya
kufutwa magazeti hayo, milango iko wazi kwa ajili ya kuwasilisha maombi mapya
ya usajili kwa kufuata taratibu zilizopo” alisisitiza Mhe. Nnauye.
Akifafanua
Mhe. Nnauye amesema kuwa wamiliki wa magazeti 473 yakiwemo Alasiri, Pambamoto,
Mipasho, Mirindimo, na Taifa Tanzania ambao viapo vyao vimefutwa, wahakikishe
kwamba hawavunji sheria kwa kuanza biashara hii ya magazeti bila kufuata
taratibu za kujisajili upya na endapo watakiuka maelekezo hayo hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Wizara
imefanya mapitio ya viapo vya usajili wa magazeti yote na Ofisi ya Waziri
mwenye dhamana ya Habari imejiridhisha kuwa kuna idadi ya magazeti 473 ambayo
yamesajiliwa lakini hayajachapishwa kwa zaidi ya miaka mitatu.
Kufuatia
hali hiyo, tangazo la serikali Na. 65 la tarehe 22 Machi, 2013 lilitolewa kwa
ajili ya kutangaza kusudio la kufuta viapo vya usajili wa magazeti 550 na
kupewa fursa ya kujitetea au kuonyesha nia ya kuendelea kuchapisha.
Baada
ya tangazo hilo magazeti 77 yalionyesha nia yakuendelea kuchapisha, kwa mantiki
hiyo hadi sasa kufuatia orodha ya wakati huo pamoja na kupewa muda mrefu zaidi
ya unaotakiwa kuna magazeti 473 ambayo hayachapishwi na yamekosa sifa ya
kuendelea kutambulika na msajili wa magazeti kwa mujibu wa sheria.
Aidha
Mhe. Nnauye ametoa pongezi kwa wamiliki wa vyombo vya habari ambao wamekuwa
wakifuata sheria na taratibu zinazosimamia tasnia ya habari ili kufikia malengo
ya kuwahudumia wananchi kwani Serikali inathamini sana mchango wa huduma
ya vyombo hivyo.
Kwa
mujibu wa takwimu za ofisi ya Msajili wa Magazeti iliyopo chini ya Idara ya
Habari (MAELEZO), Tanzania inayo magazeti na majarida 881 yaliyosajiliwa
kisheria. Hata hivyo licha ya magazeti na majarida kusajiliwa yapo baadhi
yameshidwa kuchapishwa na wamiliki mara baada ya kusajiliwa na mengine
yalichapishwa kwa muda mfupi na kuacha kabisa uchapishaji.
Picha: Genofeva Matemu –
WHUSM
No comments