TANZANIA KUNUFAIKA NA MPANGO WA MAENDELEO WA MATTEI KWA USHIRIKIANO NA UNDP
Roma, Italy - Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ameshiriki katika mjadala wa ngazi ya juu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) jijini Roma, Italia ukilenga kufungua fursa za maendeleo endelevu kwa Afrika.
UNDP imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na Tanzania kupitia ofisi zake nchini na hivyo kwa kushirikiana na Mpango wa Maendeleo kwa Afrika wa Mattei ni dhahiri Tanzania itanufaika kwa ushirikiano mzuri baina yake na Italia katika kubadilishana taaluma na ujuzi katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha kuwa mpango huu unawiana na vipaumbele vya Taifa.
Akizungumza katika mjadala huo, Mhe. Kombo alisema "Tunataka wote tunufaike," ili huu uwe ushirikiano ambao unanufaisha wawekezaji wa Italia na Watanzania. Tanzania tayari imewasilisha mapendekezo ya maeneo ya ushirikiano baina yake na Italia kupitia mpango wa maendeleo wa Mattei ambayo yanajumuisha eneo la mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, nishati safi, uchumi wa buluu, mifugo na uvuvi, pamoja na kilimo cha kahawa. "Tunaamini kahawa inaweza kuongeza thamani kubwa kupambana na mabadiliko ya tabianchi," Mhe. Kombo amebainisha, akieleza uzalishaji endelevu wa kahawa utachangia ukuaji wa uchumi na ulinzi wa mazingira.
Waziri Kombo anasisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika miradi yote ya kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na mipango ya mazingira ikiwemo ulinzi wa vyanzo vya maji vya Tanzania dhidi ya ‘microplastics’ na athari zake. Shirika la UNDP la Vijana wanaopambana na mabadiliko ya Tabianchi (Youth for Climate -Y4C) linawaleta pamoja vijana kutatua changamoto za tabianchi.
“Kwa pamoja tukiitunza Dunia, Dunia nayo itatutunza sote,” Mhe. Kombo alihitimisha, akisisitiza umuhimu wa hatua za pamoja katika kutatua changamoto za kimataifa.
Nchi nyingine za Afrika zikiwemo; Zambia, Angola, na DRC zilishiriki katika majadiliano haya.
Post Comment
No comments