MAJALIWA: VETA ENDELEENI KUJIIMALISHA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA DUNIANI
Na Neema Mpaka, Dar es salaam - Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amehimiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuendelea kujiimarisha ili kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani kwa kutoa mafunzo yanayojumuisha ujuzi wa kisasa unaochochea uzalishaji wenye tija.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es salam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 30 ya VETA ambapo amesema kuwa taasisi za elimu na mafunzo ya ufundi zinatakiwa kwenda kuhakikisha mitaala yao inaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
"Serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa lazima tushirikiane kufanya tafiti mara kwa mara ili kujua ni ujuzi gani unahitajika sokoni na kuhakikisha wahitimu wetu wanakuwa na maarifa sahihi," amesema Majaliwa.
Aidha amesema takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinaonyesha kuwa ajira nyingi duniani zinapatikana kwenye sekta binafsi na zinahitaji elimu ya ufundi stadi, hususan katika kilimo, ujenzi, usafirishaji, na huduma za kijamii.
waziri majaliwa ameongeza kuwa kati ya ajira milioni 7 zilizozalishwa nchini kati ya mwaka 2020 na 2024, ajira katika sekta isiyo rasmi zilifikia milioni 6.1 (asilimia 87.1), huku sekta rasmi ikiajiri takribani watu 907,873 (asilimia 12.9).
"Nitoe wito kwa wizara husika kushirikiana kuhakikisha vyuo 65 vya ufundi vinavyojengwa na Serikali vinakamilika haraka, ili kupanua wigo wa elimu ya ufundi kwa vijana. Kukamilika kwa vyuo hivyo kutaifanya VETA kuwa na jumla ya vyuo 145 nchini."Amesema Majaliwa
Amesema Kuna umuhimu wa utoaji wa taarifa kwa wananchi kuhusu fursa za mafunzo, kwa kuwa kuna vijana wengi wa vijijini ambao huenda hawajui kuhusu nafasi zinazopatikana.
Kwa upande wake Waziri wa elimu Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema kuwa katika kuadhimisha siku hii veta imejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza na kuendeleza uchumi kupitia ufundi stadi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema mamlaka hiyo itaendelea kuboresha mafunzo na kusimamia utoaji wa ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira ili kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanakuwa na fursa bora za kujiajiri na kuajiriwa.
Post Comment
No comments