WAFANYABIASHARA 1520 KUSAJILIWA AWAMU YA KWANZA SOKO LA KARIAKOO - HAWA GHASIA
Dar es salaam - wenyekiti wa Bodi ya Shirika la Masoko ya Kariakoo Hawa Ghasia amesema kuanzia Januari 31 mwaka huu wanaanza kuweka majina ya wafanyabiashara 1,520 ambao walikuwepo kwenye soko la Kariakoo kabla ajali ya moto ya Julai 10, 2021 ili wasajiliwe kwenye mfumo wa TAUSI.
Akizungumzia juu ya wafanyabiashara wapya bi. Ghasia alieleza kuwa taarifa rasmi ya nafasi za biashara kwenye soko hilo itatangazwa mara baada ya kuwapanga kundi la kwanza la waliokuwepo.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo alisema, hakuna mfanyabiashara ambaye atarejeshwa sokoni kabla hajalipa deni la awali. Alitaja kuwepo kwa wafanyabiashara 366 wanaodaiwa zaidi ya shilingi Milioni 358 za awali kabla ya soko kuungua, hivyo akatoa wito wakiona majina yao wafanye utaratibu wa kulipa kabla hawajapatiwa funguo za kurejea sokoni.
Soko la Kariakoo lilisitisha shughuli zake mwaka 2021 mara baada ya ajali ya moto na sasa serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha kutumia shilingi Bilioni 28.03 kulikarabati na kujenga lingine ambalo litaanza kazi rasmi mwezi Februari mwaka huu.
Mapema akizungumzia mchakato huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Albert Chalamila alitangaza kuwa kuanzia Februari 22 mwaka huu biashara katika soko la Kariakoo zitaanza kufanyika kwa muda wa masaa Ishirini na Nne.
"Dar es Salaam sasa ianze kufanya biashara saa 24 kuanzia tarehe 22 Februari mwaka huu ambapo ufunguzi utafanyika. Eneo la uzinduzi litaanzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hadi Kariakooo ambapo maeneo yote yatakuwa na ulinzi na taa za uhakika" alisisitiza RC Chalamila.
No comments