Breaking News

BRELA YAZIFUTIA USAJILI KAMPUNI 11 KWA KUKIUKA MASHARTI YA USAJILI

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) bwana Godfrey Nyaisa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari mapema leo march 5, 2025 jijini Dar es Salaam.

Dar es salaam - Msajili wa Kampuni amefuta Kampuni 11 kwa kukiuka masharti ya usajili kifungu cha 400A (1) (e) cha Sheria ya Kampuni Sura 212 kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika Katiba za Kampuni hizo na miongozo ya Uendeshaji wa Kampuni wakati wa usajili.

Akizungumza mapema leo Machi 5, 2025 jijini Dar ea salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) bwana Godfrey Nyaisa amesema kampuni hizo zimekiuka masharti kwa kufanya shughuli za kibiashara tofauti na madhumini yaliyoainishwa katika katiba za kampuni na miongozo ya uendeshaji wake wakati wa usajili.

"Kwa mujibu wa Sheria Kifungu hiki kikikiukwa Msajili anatakiwa kuchukua hatua chini ya kifungu 400A (1) (e) ambazo ni kuijulisha Kampuni kuhusu ukiukwaji na hatua anazokusudia kuzichukua kwa Kampuni husika,". Alisema Bw  Nyaisa na kuongeza,

"Sheria inaendelea kueleza kuwa, endapo Kampuni itashindwa kutoa maelezo, au kutoa maelezo yasiyoridhisha, Msajili atafuta Kampuni husika kwenye Rejista ya Kampuni,".

Aidha Bw. Nyaisa amebainisha kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 400A (1) (e) Msajili alizijulisha Kampuni husika kuhusu kusudio la kuzifuta kupitia notisi zilizotolewa kati ya Januari 2 na 26 Mwaka huu.

Sambamba na notisi hiyo Kampuni hizo hazikuwasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu 400A (2), Msajili amezifuta rasmi Kampuni hizo kuanzia Februari 27 Mwaka huu ambazo ni LBL Mtwara Media Company Limited (Na. 181289972) na LBL Morogoro Media Company Limited (Na. 179770873).

Nyingine ni LBL Geita Advertising Media Limited (Na. 180439242), LBL Mbeya Media Limited (Na. 179978326), LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited (Na. 181302259) na LBL Mbezi Advertising Media Company Limited (Na. 180582835).

Bwana Nyaisa amezitaja Kampuni nyingine kuwa ni LBL Ubungo Media Limited (Na. 180960333), LBL Mabibo Media Company Limited (Na. 181117346), LBL Mbagala Media Company Limited (Na. 181248874), LBL Gongo la Mboto Media Advertising Limited (Na. 181513438) na LBL Dar es Kigamboni Advertising Company Limited (Na. 180046992).

"Msajili anapenda umma ufahamu kwamba, hakuna Sheria wala Taasisi yenye Mamlaka ya kutoa vibali wala leseni za kufanya biashara za upatu za upatu hapa Nchini,". Alisema Bw.Nyaisa na kiongeza kuwa

"Msajili anaendelea na ufuatiliaji wa Kampuni nyingine zinazofanya shughuli za biashara nje ya Katiba zao na kinyume na Sheria na taratibu na ataendelea kuzichukulia hatua stahiki ikiwemo kuzifuta kwenye Rejista ya Kampuni".

Aidha amesisitiza kuwa biashara ya upatu ni kinyume na Sheria za Nchi, hivyo nitoe rai kwa Wananchi kutoa taarifa mara Moja Kwa Mamlaka husika zikiwemo Taasisi za kiserikali na Jeshi la Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya Kampuni au watu kunaojihusisha na biashara hiyo.

No comments