Breaking News

KAMISHNA DORIYE AWATAKA WATUMISHI WA NCAA KUONGEZA UBUNIFU

 

Na Mwandishi wetu - Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kuongeza ubunifu katika utendaji wao wa kazi wa kila siku ili kuongeza mapato na hivyo kusaidia kuimarisha huduma za uhifadhi,utalii na maendeleo ya jamii.

Kamishna Doriye ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo katika makao makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mjini Karatu.

Ameeleza kuwa sekta ya utalii kwa sasa inahitaji ubunifu wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na kubuni mazao mapya ya utalii pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wageni wanaotembelea vivutio mbalimbali.
“Dunia imebadilika na wageni wanachohitaji ni kupata huduma zilizo bora, ni jukumu letu kuongeza ubunifu ili tuweze kuongeza mapato na hivyo kuboresha huduma zetu za uhifadhi na utalii”, alisema Dkt. Doriye.

Katika kikao hicho Dkt. Doriye amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa kujituma, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kushirikiana na kutumia rasilimali za mamlaka hiyo katika kufanikisha malengo yaliyowekwa na serikali katika kusimamia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.

Katika kikao hicho watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wamempongeza Kamishna Doriye kutokana na utendaji kazi wake ambapo kwa muda mfupi tangu ateuliwe kushika wadhifa huo amewezesha kurudisha ari ya watumishi kufanya kazi, mshikamano na kusimamia vema ukusanyaji wa mapato.
Watumishi hao wamesema kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa sasa inaonekana kubadilika kiutendaji kutokana na watumishi kupata stahiki zao kwa wakati jambo ambalo limeongeza ari ya kufanya kazi, ushirikiano pamoja na upendo.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wafanyakazi wa mamlaka hiyo kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Amboni, Songwe na Handeni.

No comments