Breaking News

KAMANDA MULIRO - JESHI LA POLISI KUENDELEA KUIMALISHA ULINZI NA USALAMA, ATAJA MAFANIKIO MWAKA 2024

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limeuanza mwaka 2025 vizuri na sherehe za Krismasi na mwaka mpya zilikuwa za amani na utulivu ikiwa ni matokeo ya kudhibiti matukio hatarishi ambapo madereva 179 walipimwa ulevi.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro amesema usimamizi wa Sheria na kanuni mbalimbali zikiwemo sheria za Usalama barabarani zilisimamiwa kikamilifu ili kudhibiti ajali za barabarani.

Katika kipindi cha sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya 2025, makosa hatarishi ambayo yangepelekea ajali yalidhibitiwa na kuchukuliwa hatua kwa wahusika; Jumla ya madereva 179 walituhumiwa na kupimwa ulevi kati yao madereva 30 walikutwa na ulevi kiwango cha zaidi ya miligramu 80. Kati yao Madereva 22 walitokea Wilaya ya Kinondoni, madereva 06 Wilaya ya Ilala na madereva 02 Wilaya ya Temeke. 

Kufuatia kuwepo kwa madereva wenye kiwango kikubwa cha ulevi, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limewafungia leseni za udereva waliokamatwa kwa kipindi cha miezi 06 kwa mujibu wa kifungu 28 (3) (b) cha Sheria Usalama barabarani sura 168 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
 
Vilevile katika kipindi cha mwezi Novemba hadi Desemba 2024, Jeshi la Polisi Dar es Salaam lilifanikiwa kupata matokeo Mahakamani ya watuhumiwa mbalimbali waliofikishwa kwenye mahakama hizo. 

Miongoni mwao ni Sadick Foreni (30) mkazi wa Mbagala katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke ilimuhukumu kifungo cha maisha jela kwa kosa la Kulawiti, mahakama hiyo ya Temeke ilimuhukumu pia Joseph Ferdinand (35) mkazi wa Mbagala Kibonde Maji kifungo cha maisha jela kwa kosa la Kulawiti.  

Ayub Hatibu (32) Mkazi wa Tabata alihukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kubaka kwenye Mahakama ya Wilaya Kinyerezi, Salmin Athuman (30) mkazi wa Kitunda alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha .

Henry Peter (36) mkazi wa Mbezi Mahakama ya Wilaya ya Ubungo alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka. Ramadan Amir (30) mkazi wa Kawe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.


Jeshi la Polisi litaendelea kujikita katika kuzuia matukio ya kihalifu kwa kufuatilia kwa karibu makundi yote ya watu wakiwemo wanaotumia dawa za kulevya na kufanya matukio ya kihalifu ambapo jumla ya watuhumiwa 250 walikamatwa kwa kuhusika na kuuza, kusafirisha na kutumia dawa za kulevya.

Aidha, Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam tarehe 17 Desemba, 2024 limemkamata Ally Ismail (22) Mkazi wa Kipunguni Mashariki kwa tuhuma ya uvunjaji, na alipatikana na vitu mbalimbali vya wizi pamoja na 
Televisheni 03, Kompyuta za mezani 03, Kompyuta mpakato 02, Ving’amuzi 04, Keyboard aina ya Dell 04, Simu janja 08, Simu ndogo 06, Camera aina samsung 01, Begi kubwa 01 lenye nyaya mbalimbali, Jiko 01, radio ,mtungi wa gesi 01, Mashine ya kunyunyuzia dawa shambani 01 na atafikishwa mahakamani

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana ili kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi ikiwa ni pamoja na kutekeleza falsafa ya ulinzi shirikishi ili kuzuia vitendo vya kihalifu. 

No comments