UJENZI WA KITUO KIKUU CHA GESI WAFIKIA ASILIMIA 80
Dar es salaam - Ujenzi wa Kituo Kikuu cha kujazia Gesi Asilia (CNG Mother Station) unaofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umefikia asilimia 80 hadi kukamilika kwake na kuelezwa kuwa mwishoni mwa mwezi Januari, 2025 kitaanza kutumika kusambaza nishati hiyo muhimu.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo Januari 6, 2025 baada ya kukagua kituo hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema awali serikali iliahidi kukamilika kwa mradi huo mnamo mwezi Desemba 2024 lakini umechelewa baada meli iliyokuwa imebeba mitambo hiyo kutoka China kuchelewa kufika nchini.
Akieleza hatua za ujenzi wa kituo hicho, Dkt. Mataragio amesema mitambo imeshasimikwa na kinachoendelea kwa sasa ni kazi ndogondogo za kuunganisha mfumo wa umeme ili kuanza kufanya kazi.
Aidha amesema hadi kufikia Januari 16, 2025, ujenzi utakuwa umekamilika na kuanza majaribio huku akiwahakikishia watumiaji wa nishati hiyo kuanza kupata huduma kituoni hapo mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu.
Ujenzi huo hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 14.5 kikijumuisha ununuzi wa magari tisa na ujenzi wa vituo viwili vya kujazia gesi kwenye magari katika maeneo ya Muhimbili Dar es Salaam na Kibaha mkoani Pwani.
Source Tbc Online
No comments