TMA YAWAHAKIKISHIA HUDUMA BORA ZA HALI YA HEWA WADAU WA USAFIRI WA ANGA
Dar es Salaam - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wadau wa usafiri wa anga wanaotumia huduma za hali ya hewa nchini na kuwahakikishia upatikanaji wa huduma bora za hali ya hewa katika sekta hiyo ya usafiri wa anga.
Aidha katika mkutano huo wadau walijadiliana namna bora ya kuendelea kuboresha huduma hizo zinazotolewa na Mamlaka. Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kufunguliwa rasmi na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia Mkurugenzi anayesimamia Ubora wa huduma za hali ya hewa Dkt. Geofrid Chikojo, tarehe 18 Desemba 2024.
“Huduma za hali ya hewa nchini hususan zinazotolewa kwenye shughuli za usafiri wa anga zimekidhi vigezo vya kimaitaifa, yaani zimethibitishwa na viwango vya ubora vya kimataifa (ISO certified). Kila mwaka Mamlaka imekuwa ikikaguliwa na wakaguzi kutoka nje ya nchi na hata Taasisi zenye dhamana hiyo nchi na matokeo yake yamendelea kubainisha ubora wa huduma zetu”. Alisema Dkt. Chikojo
Awali, Dkt. Chikojo alieza lengo la mkutano huo ni kujadiliana ana kwa ana, kupokea maoni ya wadau hao pamoja na kufafanua uboreshaji wa huduma zitolewazo na Mamlaka kutokana na uwekezaji mkubwa unaendelea kufanywa na Serikali kwenye miundombinu na wataalamu kwa ujumla.
”Kwa kipindi cha miaka hii mitatu Mamaka imefanikiwa kufunga rada mbili za hali ya hewa, hivyo kuongeza idadi ya mtandao wa rada nchini na kufikia 5 katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Mbeya na Kigoma. Aidha, Mamlaka imefunga mitambo maalum katika viwanja zaidi ya 10 nchini, mitambo ambayo inasaidia kutoa taarifa muhimu za hali ya hewa kwa ajili ya kusaidia usafiri wa ndege wakati wa kutua na kuruka”. Alizungumza Dkt. Chikojo.
Naye Rubani Busee S. Busee, mdau kutoka Ndege za Serikali, aliipongeza TMA kwa kuendelea kuboresha huduma zake kwa kuwezesha usalama wa utendaji kazi wao. Aidha aliiomba Mamlaka kuhakikisha huduma zinaenda sambamba na teknolojia ya kisasa.
No comments